Header Ads Widget

TAKUKURU YAJIPANGA KUDHIBITI MAPUNGUFU KWENYE MIRADI





Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa Kigoma imesema kuwa itaendesha mafunzo, semina na kufanya vikao na wasimamizi wa miradi katika ngazi za kata na Halmashauri ili kukabiliana na mapungufu yanayojitokeza katika utekelezaji wa miradi.

 

Mkuu wa dawati la elimu kwa Umma TAKUKURU mkoa Kigoma,Ibrahim Sadick alisema hayo akitoa ufafanuzi kuhusiana na taarifa ya kila robo mwaka inayotolewa na taasisi ambapo waandishi walitaka kujua hatua wanazochukua kutokana na taarifa kuonyesha kujirudia  kwa makosa yanayotokea kwenye utekelezaji wa miradi.

 

Sadick alisema kuwa katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza hatua ya awali ambayo TAKUKURU itachukua ni kutoa elimu kwa wasimamizi wote wanaohusika na miradi wakiwemo Madiwani, wataalam wa Halmashauri, kamati za usimamizi wa miradi za kata,walimu wakuu na watendaji wa kata.

 

Maelezo hayo ya Mkuu wa dawati la elimu kwa umma TAKUKURU mkoa Kigoma yanakuja kukiwa na taarifa ya utekelezaji ya taasisi hiyo katika kipindi cha   robo mwaka kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu ikionyesha kuwepo kwa  jumla ya miradi 35 yenye thamaani ya shilingi Bilioni 18.6 ambayo ilifanyiwa mapitio na  kati yake miradi 19 yenye thamani ya shilingi Bilioni 7.7 ilikutwa na mapungufu.

 

Katika taarifa iliyotolewa na Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa Kigoma, John Mgallah ilianinisha  mapungufu hayo kuwa ni pamoja na kutozingatiwa kwa sheria za manunuzi, kutozingatiwa kwa taratibu za ujenzi ikiwemo kutozingatiwa kwa ramani za majengo, kuchelewa kwa miradi na baadhi ya nyaraka muhimu za utekelezaji wa miradi ikiwemo mihutasari ya kutoa fedha, nyaraka za kupokea vifaa kutoonekana.


John Mgallah Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa Kigoma


Ibrahim Sadick Mkuu wa dawati la elimu kwa umma TAKUKURU mkoa Kigoma

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI