Na Rehema Abraham
Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini amewasihi wananchi wa Kata ya Kibosho Kirima kuchagua Viongozi wenye uwezo wa kushughulika na changamoto zao kwa urahisi ambao kiuhalisia wanatokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alisema, wakIfanya hilo bila shaka yoyote watapata maendeleo ya haraka katika jamii yao.
Profesa Ndakidemi ameyasema hayo tarehe 26 Novemba, 2024 wakati akihitimisha kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Kata ya Kibosho Kirima zilizofanyika katika Kijiji cha Boro ambako amezaliwa. Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika kesho tarehe 27 Novemba, 2024.
Amesemema kuwa, CCM ndicho chama pekee kinachojua changamoto za watu wa Boro na kinao uwezo wa kuzitatua kwakuwa kwa dhamana CCM iliyopewa kupitia Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweza kuzishughulikia hivyo ni vyema kuendelea kukiamini ili kuzimaliza zote. "Ndugu wanakijiji wenzangu, nipeni viongozi wa Kijiji hiki kupitia CCM kwa kura nyingi za ndiyo ili nitembee kifua mbele kwenda kuwaombea miradi ya maendeleo". Alisema Profesa Ndakidemi.
Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Kijiji ndugu Laurent Mushi amesema wakimpatia ridhaa ya kuongoza Kijiji cha Boro anakotoka Mbunge, atahakikisha suala la ulinzi na usalama analitekeleza ili wananchi waishi kwa amani. Pia alisema, atawasaidia vijana ili washikamane na kujiletea maendeleo, kwa kupatiwa mikopo ya vijana iliyotolewa na mama Samia. Pia aliahidi kuzipigania kaya masikini Kijijini ili wanufaike na TASAF.
Mushi ameomba wananchi wamchague pamoja na wenyeviti wa vitongoji na wajumbe wote ili waweze kuwasimamia na kusikiliza kero zao, na baadaye wawaletee maendeleo.
Mwenyekiti wa CCM kata ya Kibosho Kirima ndugu Patrick Lazaro Mushi akifunga kikao kwenye hizo kampeni alitoa wito kwa wanakijiji wote wahamasishane na kujitokeza kupiga kura kwa wingi kwani ushindi kwa CCM ni muhimu sana kwa maslahi ya Kijiji Cha Boro.
Katika hadhara hiyo, Mheshimiwa Ndakidemi alimpokea mwanachama mpya kutoka CHADEMA ambaye ni mwanamama mfanyabiashara maarufu kutoka kijiji cha Boro.
0 Comments