Na Matukio Daima App - Pwani
Jeshi la polisi mkoa wa Pwani linawashikilia Wafanyakazi wa kampuni ya mikopo ya OYA kwa tuhuma za mauaji ya Juma Said Mfaume kwa kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili mume wa mdaiwa wao Khadija Ramadhani huko Mlandizi Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani ACP Muhudhwari Msuya Ofisini kwake Kibaha mkoani Pwani amesema tukio limetokea Oktoba 7 mwaka huu katika kitongoji cha Mbagala Wilaya ya kipolisi Mlandizi ambapo Wafanyakazi hao wa kampuni ya mikopo ya OYA walifika nyumbani hapo kwa lengo la kudai fedha za marejesho ya mkopo kwa make wa Juma Said Mfaume aitwaye Khadija Ramadhani.
Baada ya kufika nyumbani kwa Juma aliwaelekeza kuwa mkewe hayupo lakini watuhumiwa hao walilazimisha kuingia ndani kwa nguvu huku wakimshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia fimbo na baadae alianguka chini na kupoteza fahamu.
Alisema kutokana na hali hiyo Watuhumiwa walimbeba Juma kwenye gari lao kumpeleka hospitali alifariki akiwa anapatiwa matibabu katika Kituo Cha afya cha Mlandizi.
"Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na daktari kisha kukabidhiwa ndugu kwa taratibu za mazishi.
Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani linatoa wito kwa makampuni na taasisi za a kifedha kufuata taratibu za kisheria katika kudai fedha kutoka kwa wateja wao ili kuepusha usumbufu na madhara yanayoweza kutoka ikiwemo uharibifu wa Mali, kujeruhi na vifo.
0 Comments