Header Ads Widget

UJENZI WA MJI WA SERIKALI MTUMBA NA FURSA LUKUKI KWA WANANCHI



Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima media,Dodoma

JIJI la Dodoma lilitenga eneo la mji wa Serikali Mtumba ambalo lipo katika Kata ya Mtumba kilomita 17 kutoka katikati ya Mji. 


Eneo hilo lina ukubwa wa hekta 617.15, sawa na ekari 1,542.88, na limepangwa kwa umakini ili kutoa huduma bora na kukidhi mahitaji ya serikali pamoja na wananchi.


Mji wa Serikali Mtumba unapakana na Kambi ya Jeshi ya Ihumwa upande wa magharibi, Kata ya Mtumba kaskazini-mashariki, na barabara kuu iendayo Dar es Salaam upande wa kusini. 


Eneo hilo limegawanywa katika sehemu mbalimbali kama vile wizara za serikali, ofisi za mabalozi, nyumba za serikali, maeneo ya biashara, huduma za jamii, pamoja na miundombinu muhimu kama Bunge, mahakama, na maegesho ya magari.

Mtumba kumejengwa kwa barabara za kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 51.2 kwa gharama ya shilingi bilioni 88.1, huku asilimia 56 ya ujenzi huo ikiwa imekamilika. 


Meshack Bandawe, aliyekuwa Katibu wa kuratibu serikali kuhamia Dodoma, alieleza kuwa ujenzi wa barabara hizo ulikamilika kwa wakati na ulihusisha njia mbili zenye urefu wa kilomita 22.4 na njia moja zenye urefu wa kilomita 28.8.


 Miundombinu mingine iliyojengwa ni pamoja na mifumo ya maji, umeme, gesi, mawasiliano ya tehama, na huduma za zimamoto na uokoaji.


Mradi huo wa barabara ulitekelezwa na kampuni ya China Henan International Cooperation Co. Ltd (CHICO) na kusimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA). 


Ujenzi huo ulizinduliwa rasmi na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, mwezi Machi 2019.


Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alionyesha juhudi kubwa na dhamira ya dhati katika kuhakikisha azma ya serikali ya kuhamia Dodoma, iliyokuwa ikizungumziwa kwa muda mrefu, inatimia. Tangia alipoingia madarakani mwaka 2015, Magufuli aliweka mkazo kwenye utekelezaji wa mpango huu kwa vitendo, akiamini kuwa ni hatua muhimu ya kuimarisha usimamizi wa serikali na kuboresha utendaji wa kiutawala.


Mnamo mwaka 2016, alitangaza rasmi kuanza kwa mpango wa serikali kuhamia Dodoma, na alihakikisha kuwa wizara zote na taasisi muhimu za serikali zinafanya hivyo. 


Ili kuhakikisha utekelezaji huo unafanikiwa, serikali ilitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu muhimu kama barabara, maji, umeme, na majengo ya ofisi za serikali katika eneo la Mtumba, lililotengwa maalum kwa ajili ya Mji wa Serikali.


Magufuli alifuatilia kwa karibu maendeleo ya mradi huu, na mnamo Machi 2019, alizindua rasmi mradi wa ujenzi wa barabara za lami ndani ya Mji wa Serikali Mtumba. 


Barabara hizo, zenye urefu wa kilomita 51.2, zilitengenezwa kwa usimamizi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na mkandarasi China Henan International Cooperation Co. Ltd (CHICO).

Juhudi hizi zilionyesha uzalendo na uthubutu wa Magufuli katika kuimarisha hadhi ya Dodoma kama Makao Makuu ya kudumu ya Tanzania. 

Hayati Magufuli Alisisitiza kuwa kuhamia Dodoma si tu kutakachowezesha serikali kufikia wananchi wake kwa urahisi, bali pia kutachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa mkoa wa Dodoma na taifa kwa ujumla.

Kwa jitihada hizo, Hayati Magufuli aliacha urithi wa maendeleo ambao umeendelea kuimarishwa na Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendeleza na kukamilisha miradi hiyo muhimu.

Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan, aliweza kuendelea na dhamira ya kuendeleza mji huo kwa kutenga zaidi ya shilingi bilioni 600 kwa ajili ya awamu ya pili ya ujenzi wa majengo ya ofisi za serikali.

Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan, alionyesha dhamira ya dhati na uongozi thabiti katika kuendeleza ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba, hatua ambayo ilianza na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Rais Samia aliweza kuendeleza miradi muhimu na kuhakikisha miundombinu ya kisasa na huduma za kijamii zinakamilika kwa wakati, ili Mji wa Serikali uweze kutumika kikamilifu na kutoa huduma bora kwa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla.


Moja ya hatua muhimu alizochukua ni kutenga zaidi ya shilingi bilioni 600 kwa ajili ya awamu ya pili ya ujenzi wa majengo ya ofisi za serikali, ikiwa ni pamoja na miundombinu ya kisasa kama maji, umeme, mifumo ya mawasiliano ya tehama, na huduma za zimamoto. 


Katika mwaka wa fedha 2021/2022, Rais Samia alitenga shilingi bilioni 300 kwa ajili ya kukamilisha majengo hayo, yanayojumuisha majengo ya ghorofa sita na zaidi, ili kuongeza uwezo wa ofisi za serikali na kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.


Rais Samia pia alihakikisha ushirikiano wa taasisi muhimu kama DUWASA (Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma), TANESCO (Shirika la Umeme Tanzania), TTCL (Kampuni ya Mawasiliano ya Simu Tanzania), na Zimamoto, katika kuhakikisha huduma zote muhimu zinapatikana kwa wakati.


Dhamira ya Rais Samia ya kuendeleza mji huo ulionekana wakipekee na kuadhihirisha nia yake ya kuendeleza maono ya serikali ya kuhakikisha Dodoma inakuwa Makao Makuu ya kudumu yenye hadhi, miundombinu bora, na huduma zinazokidhi mahitaji ya serikali na wananchi. 


Kwa juhudi hizo, Rais Samia alionyesha uzalendo na uongozi thabiti katika kuimarisha na kuboresha huduma za umma, huku akichochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla.

 Jenista Mhagama, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, alisema kuwa tangu serikali ilipotangaza azma ya kuhamishia shughuli zake Makao Makuu Dodoma mwezi Septemba 2016, watumishi 18,300 walihamia Dodoma ifikapo Juni 2021, na shilingi bilioni 655 zilitumika kuhamisha watumishi na kujenga ofisi za awali za wizara 23.

Waziri huyo kwa wakati ule alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza maono ya serikali na kukubali mpango mkakati wa ujenzi wa majengo ya ofisi za serikali awamu ya pili, ambapo majengo ya ghorofa sita na zaidi yatatumika. 

Utekelezaji wa mradi huo ulijumuisha taasisi mbalimbali kama DUWASA, TANESCO, TTCL, Zimamoto, NEMC, OSHA, TFS, na GSO. Kamati maalum za ufuatiliaji na usimamizi ziliendelea kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu maendeleo ya ujenzi na changamoto zilizojitokeza ili kutafuta suluhisho la haraka na kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi.

Wananchi wanaoishi Mtumba wameshukuru kwa juhudi hizo za serikali. Janeth Kusena, mkazi wa Mtumba, alisema kuwa ujenzi wa mji huo umeleta maendeleo makubwa, na eneo hilo sasa limepanda hadhi. “

Awali, Mtumba ilikuwa ni pori na hakukuwa na maendeleo, lakini sasa wakazi wanauwezo wa kuuza maeneo yao kwa bei nzuri kutokana na ujio wa mji wa serikali,” alisema.

Pia, Pisi Mazengo, mkazi wa Mtumba Mogamboga, alisema kuwa usafiri umeimarika, na wakazi wanaweza kusafiri kwa urahisi na haraka bila changamoto za usafiri kama ilivyokuwa awali. 


“Sasa tunaweza kufika mjini na kurudi muda wowote bila shida, na kwetu ni neema kubwa,” alieleza.


Yohana Yohana, mfanyabiashara wa usafirishaji katika mji wa Mtumba, alionyesha furaha yake kwa mabadiliko haya. Alisema kuwa ongezeko la abiria limeboresha biashara yake na sasa ana uwezo wa kujipatia kipato cha kutosha.

 “Nashukuru serikali kwa kutuletea mji huu, umetusaidia hata sisi wa hali ya chini kujenga maisha kupitia biashara zetu,” alisema.

Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba umeleta mabadiliko makubwa, si tu kwa miundombinu ya serikali, bali pia kwa wakazi wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla. 

Uamuzi wa kuhamishia shughuli za serikali Dodoma unadhihirisha nia ya dhati ya serikali kuendeleza taifa na kuboresha maisha ya wananchi wake. Wananchi wameanza kuona matokeo chanya ya mradi huu, na matumaini yao yanaendelea kuongezeka kadri maendeleo yanavyosonga mbele.

Mji wa Serikali Mtumba ni alama ya maendeleo na mfano wa mafanikio ya serikali katika kujenga taifa imara lenye huduma bora kwa wananchi wake. Serikali inaendelea kuonyesha dhamira ya dhati katika kuhakikisha Dodoma inakuwa kitovu cha utawala na maendeleo ya kiuchumi nchini.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI