Na Fatma Ally Matukio Daima App, Dar
Serikali imesema inatambua uzingatiaji wa masuala ya jinsia kuwa una mchango mkubwa katika kukuza ustawi wa wananchi na maendeleo ya taifa, hivyo imeweka msisitizo mkubwa katika kukuza usawa wa kijinsia katika kufanya maamuzi katika ngazi zote, ikiwa ni pamoja na Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Taasisi za Umma na Binafsi, Asasi za Kiraia pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Waziri wa Maendeleo ya Jamii Wazee na Watoto, Zanzibar Riziki Pembe Juma kwenye amesema kongamano la wanawake katika Uongozi la mwaka 2024 lina dhima ya “Umuhimu wa Uongozi wa Mabadiliko kwa Viongozi Wanawake Barani Afrika”, ambapo mada hiyo ni muhimu katika kumjenga mwanamke.
Amesema kuwa, jitihada mbalimbali zimefanyika ili kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa katika michakato ya uandaaji na utekelezaji wa mipango ya rasilimaliwatu, ajira, mafunzo, upandishwaji vyeo, ubadilishwaji vyeo/kada, urithishanaji wa madaraka na uteuzi katika nafasi mbalimbali za uongozi na maamuzi katika taasisi za umma ili kupunguza tofauti za uwakilishi kati ya wanawake na wanaume katika vyombo mbalimbali vya maamuzi.
"Katika kufanikisha hayo yote, Serikali inatekeleza sera, mikakati na mipango mbalimbali ya maendeleo, kwa mfano Serikali inatekeleza Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000 pamoja na Mkakati wake wa 2005, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa (2021/22-2025/26) na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
Vilevile, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya Mwaka 2050, Mpango wa Tatu wa Maendeleo na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA III), Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030 pamoja na sera na mikakati mbalimbali ili kuimarisha usawa wa kijinsia na kuleta maendeleo jumuishi kwa wananchi wa Zanzibar.
Ameongeza kuwa, ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi na uongozi ni moja ya vipaumbele vya Serikali katika kuhakikisha usawa kati ya wanaume na wanawake, Takwimu zinaonyesha kuwa wanawake katika nafasi za uongozi wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na wakurugenzi katika taasisi mbalimbali za umma ni asilimia 28.6 ya viongozi wote.
Hata hivyo, amesema kongamano hilo pia litatoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya kuimarisha uongozi wa mabadiliko, hasa miongoni mwa viongozi wanawake, kwa kuzingatia umuhimu wa mjadala huu, Wizara inaomba kupokea ripoti ya Kongamano hili kwa ajili ya rejea
"Nimefahamishwa kuwa mchakato wa kujiunga na programu hii ulikuwa na ushindani mkubwa na baadhi yenu mmebahatika kuchaguliwa kuwa sehemu ya programu hii. Tunatumaini kuwa mtaipa uzito unaostahili na mtaongeza juhudi katika kujifunza na kushirki hatua zote za programu hii kwa kipindi chote cha miezi sita (6)".
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Institute Kadari Singo, kuwa hilo ni Kongamano la nne (4) ambalo ni sehemu ya uzinduzi wa mafunzo ya awamu ya tano na sita kwa viongozi wanawake ambao wamejumuika nao.
Amesema pia kongamano hilo mapoja na mambo mengine ni sehemu ya programu ya wanawake katika uongozi lenye lengo la kujadili mada mbalimbali kwa lengo la kubadilishana uzoefu na maarifa katika masuala ya uongoz
Amesema kuwa sasa wanaingia darasa la tano na sita, huku kukiwa na mwitikio mkubwa wa kushiriki kwani zaidi ya wanawake 1,500 waliomba kushiriki lakini nafasi zilizopo 100.
Singo amefafanua kuwa mafunzo hayo yanatolewa bure kwa washiriki, hivyo wanaendelea kutafuta wafadhili ili kuongeza idadi ya washiriki kila mwaka
Aidha amesema kuwa kongamano hilo limekutanisha wanawake viongozi kutoka nchi mbalimbali za barani Afrika wakiwa na lengo ni kujadili pamoja kuhusu wanawake na uongozi.
Singo amesema kuwa kongamano hilo linafanyika kila mwaka, huku akieleza kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya uongozi umeonesha wanawake wengi wapo katika nafasi za chini za utendaji.
"Tumeanzisha program hii ili wanawake wawe na sifa za juu ambazo zitawafanya kuingia katika nafasi za maamuzi, tumeanza kutoa mafunzo tangu mwaka 2022 na kufanikiwa kuhitimu wanawake 199 mpaka sasa" amesema Singo.
0 Comments