NA MATUKIO DAIMA MEDIA
Jeshi la Polisi limeeleza sababu ya kuwashikilia makada wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa ni madai ya kuvamia vituo vya kuandikisha wananchi katika Daftari la Wakazi na kufanya fujo.
Taarifa iliyotolewa juzi na Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime, ilieleza kuwa Mwenyekiti wa Jimbo la Iringa, Frank Nyalusi, alikamatwa Oktoba 20, 2024, baada ya kutembelea vituo vya kuandikisha wananchi na kulazimisha apewe madaftari hayo.
DCP Misime alisema kabla ya kukamatwa, Nyalusi alitakiwa ajisalimishe polisi, lakini alikaidi, na hivyo askari walilazimika kumkamata.
“Taarifa zinazodai kuwa kiongozi huyo alipigwa na polisi baada ya kukamatwa si za kweli. Tunatoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa hizo ambazo zinalenga kuchochea hisia za uongo,” alisisitiza Misime.
Aidha, Misime alithibitisha kukamatwa kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Katavi, Rhoda Kunchela, Oktoba 19, baada ya kudaiwa kuvamia karani wa uandikishaji wapigakura katika kijiji cha Songambele, Mlele, na kumnyang'anya daftari.
“Tulianza uchunguzi mara baada ya kupata taarifa kutoka kwa aliyedhulumiwa na mashahidi. Tumewakamata wahusika na kuwafikisha kituoni kwa hatua zaidi za kisheria,” alisema DCP Misime.
Aliwataja wengine waliokamatwa kuwa ni Festo Mgombele, Juma Masoud, Melkio Melkiades, Meshack Konja, na Nsajigwa John. Jeshi la Polisi limeonya kuwa litachukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayefanya uhalifu kwenye vituo vya uandikishaji.
LHRC Yalaani
Wakati huo huo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani kutekwa na kupigwa kwa Katibu Mwenezi wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) Taifa, Aisha Machano, kikisisitiza kuwa vitendo hivyo vinakiuka mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga, alisema: “Tunataka vyombo vya dola vichukue hatua dhidi ya wahusika kwa mujibu wa sheria. Haki lazima izingatiwe katika mchakato huu wa uchaguzi.”
Aliongeza kuwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwemo kunyanyasa wanawake wanaojihusisha na siasa, haviwezi kufumbiwa macho.
“Ni jambo la kusikitisha kwamba jana, Oktoba 21, ambayo ni Siku ya Haki za Binadamu Afrika, tunaadhimisha huku kukiwa na matukio ya uvunjifu wa haki,” alisema Dk. Henga.
Kwa mujibu wa LHRC, vitendo vya unyanyasaji vinavyolenga wanawake kwenye kipindi cha uchaguzi havikubaliki na vinapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
0 Comments