Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), mnamo tarehe 13 Oktoba 2024, tulizindua rasmi ushiriki wa wanahabari katika Samia Kalamu Awards zenye kaulimbiu "Uzalendo Ndio Ujanja."
Tunapenda kuwataarifu waandishi wa habari, vyombo vya habari, maafisa habari, na wadau wa sekta ya habari kwamba muda wa kuwasilisha maombi ya kushiriki katika tuzo hizi umesogezwa mbele hadi tarehe 30 Oktoba 2024. Awali, tarehe ya mwisho ilikuwa 26 Oktoba 2024, lakini muda umeongezwa ili kutoa nafasi kwa wale waliokumbana na changamoto mbalimbali za kiufundi, kama matatizo ya mtandao na kushindwa kupakia kazi mitandaoni.
Lengo la Tuzo
Tuzo hizi zinawalenga wanahabari wa Kitanzania kwa madhumuni ya:
Kuhamasisha na kukuza uandishi wa habari za ndani.
Kupanua wigo wa utangazaji na uchapishaji kupitia vyombo vya habari vya asili na mitandaoni.
Kuchochea uandishi wa makala za kina zinazojikita kwenye maendeleo, uwajibikaji, mila na tamaduni.
Kujenga chapa na taswira chanya ya Tanzania.
Wito kwa Washiriki
Tunaendelea kuwasihi waandishi wa habari kuchukua hatua haraka na kuwasilisha kazi zao kabla ya tarehe mpya ya mwisho, 30 Oktoba 2024. Hii ni fursa muhimu kwa wanahabari na maafisa habari kuonesha ubunifu na umahiri wao katika taaluma ya uandishi.
Kazi zote zinazowasilishwa zinapaswa kuwa za kipekee, zisizokuwa zimewasilishwa kwenye mashindano mengine, na zifuate taratibu za haki miliki. Maombi yanapaswa kuwasilishwa kupitia tovuti rasmi ya tuzo, www.samiaawards.tz.
Takwimu za Maombi
Kufikia tarehe 23 Oktoba 2024, mfumo ulikuwa umepokea maombi kutoka mikoa 23 ya Tanzania, ambayo ni:
Dar es Salaam, Dodoma, Shinyanga, Mwanza, Mtwara, Simiyu, Geita, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma, Tabora, Kagera, Mjini Magharibi, Ruvuma, Lindi, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro, na Pwani.
Mchakato wa Upigaji Kura
Upigaji kura kwa wananchi utaanza rasmi tarehe 08 Novemba 2024. Tunawataka wanahabari kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki kwa wingi katika zoezi hili, kwani asilimia 60 ya alama za mshindi zitatokana na kura za wananchi, huku asilimia 40 zikiamuliwa na jopo la majaji.
Wananchi watapiga kura kupitia SMS kwa SHORT CODE 15200 au kwa kutumia tovuti rasmi ya tuzo, www.samiaawards.tz.
Samia Kalamu Awards ni jukwaa la kipekee kwa wanahabari kuonesha mchango wao katika maendeleo ya taifa na kuimarisha ufanisi wa sekta ya habari. Tuzo hizi zinalenga kuendeleza uandishi wenye maadili, weledi, na uzalendo. Tunatoa wito kwa wanahabari kutumia fursa hii kushiriki kikamilifu, na kwa wananchi kushiriki katika upigaji kura kuanzia tarehe 08 Novemba 2024.
Imetolewa na:
Dkt. Rose Reuben
Mkurugenzi Mtendaji - TAMWA
Dkt. Jabiri Bakari
Mkurugenzi Mkuu – TCRA
0 Comments