NA JOSEA SINKALA.
Kutokana na hamasa ndogo ya wananchi kwenda kujiandikisha, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Katavi, kimefanya ziara katika maeneo mbalimbali ya mikusanyiko ya watu na kuhimiza wananchi kujitokeza kujiandikisha ili kupata haki ya kwenda kuchagua viongozi wanaowataka wakati utakapowadia (Oktoba 27, 2024).
Akizungumza na wafanyabiashara mbalimbali mjini Mpanda mkoani Katavi, mwenyekiti wa CHADEMA mkoani humo Rhoda Kunchela, amesema ni haki ya kila mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 18 kujiandikisha ili kuchagua viongozi bora.
Amesema uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji ni muhimu kwani ndio msingi wa ujenzi wa Serikali kabla ya Serikali kuu hivyo kueleza umuhimu wa wananchi kuungana kuchagua viongozi bora kwa maendeleo yao wakianza na hatua ya kujiandikisha kwa muda uliosalia hadi Oktoba 20 mwaka huu.
Kiongozi huyo amepita maeneo ya masokoni na kuzungumza na wananchi mbalimbali na kuwaasa ambao bado hawajajiandikisha kuhakikisha wanajiandikisha badala ya kukata tamaa kwa maelezo kuwa kura yao ndio itaamua maendeleo yao.
CHADEMA mkoani Katavi kinaendelea kuhimiza wananchi kujiandikisha ili kuchagua viongozi wanaowataka ikiwa zoezi hilo linatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 20, 2024 kupisha uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji Oktoba 27, 2024.
0 Comments