SEKTA ya Utalii nchini Tanzania ni mojawapo ya sekta muhimu za kiuchumi, ikitoa mchango mkubwa katika Pato la Taifa kupitia fedha za kigeni, uwekezaji, na ajira. Sekta hii inachangia zaidi ya asilimia 17 ya Pato la Taifa (GDP) na ajira takriban milioni 1.54, moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Tanzania imeendelea kuvutia watalii wa kimataifa kwa mafanikio makubwa, ikivunja rekodi za awali kabla ya janga la UVIKO-19 mwaka 2019. Kwa mujibu wa Ripoti ya Nusu Mwaka ya Takwimu za Utalii ya Shirika la Utalii Duniani (UNWTO), kuanzia Januari hadi Julai 2024, Tanzania imeshika nafasi ya kwanza barani Afrika kwa kuongezeka kwa idadi ya watalii wa kimataifa.
Aidha, Tanzania imekuwa nchi ya sita duniani kwa kuwa na ongezeko la asilimia 49 la watalii, ikitanguliwa na Qatar.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Pindi Chana, anasema ukuaji wa sekta ya utalii umetokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameongoza mageuzi makubwa kupitia programu ya Tanzania-The Royal Tour na Amazing Tanzania, pamoja na kuboresha miundombinu ya utalii nchini.
Kutokana na jitihada hizi, Tanzania imepokea tuzo nne za World Travel Awards mwaka 2024 katika vipengele vifuatavyo: kama Kivutio Bora cha Utalii Afrika – Mlima Kilimanjaro,Hifadhi Bora ya Taifa Afrika – Hifadhi ya Serengeti,Kituo Bora cha Utalii Afrika – Tanzania,Bodi Bora ya Utalii Afrika – Bodi ya Utalii Tanzania (TTB)
Dkt. Chana anasema kuwa tuzo hizi zimekuwa na faida kubwa katika kuvutia watalii, kukuza pato la taifa, kuimarisha uhifadhi wa vivutio vya utalii, na kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya utalii nchini.
Kuvutia Watalii Wengi Zaidi, Tuzo hizi zinatangaza Tanzania kimataifa kama kituo bora cha utalii barani Afrika, hatua inayoweza kuvutia watalii zaidi, hususan kutoka masoko ya kimkakati.
Kuongeza Pato la Taifa, Ongezeko la watalii linaenda sambamba na kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni, ambazo zinasaidia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama uboreshaji wa miundombinu, afya, na elimu.
Kuongeza Fursa za Ajira,Sekta ya utalii hutoa fursa nyingi za ajira, ikihusisha sekta binafsi katika huduma za malazi, migahawa, usafirishaji wa watalii, na huduma nyinginezo. Waziri Chana anasema ushindi huu utaongeza fursa zaidi za ajira, na hivyo kuongeza vipato vya kiuchumi kwa wananchi.
Kuimarisha Shughuli za Uhifadhi Kutambuliwa kwa vivutio kama Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Serengeti kumelenga kuhamasisha uhifadhi wa rasilimali za utalii. Serikali inasisitiza kuwa itaendelea kusimamia sera za uhifadhi endelevu ili kulinda vivutio vya utalii kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Kuimarisha Ushirikiano na Bodi Nyingine za Utalii, Ushindi wa tuzo ya Bodi Bora ya Utalii Afrika umeimarisha uhusiano kati ya TTB na bodi zingine za utalii duniani. Hii itasaidia katika kuweka mikakati madhubuti ya kutangaza utalii wa Tanzania kimataifa.
Kuongeza Uwekezaji katika Sekta ya Utalii ,Ushindi wa tuzo hizi unatoa ujumbe kwa wawekezaji kuwa sekta ya utalii nchini Tanzania inaendelea kukua na ina fursa nyingi za kibiashara. Waziri Chana amesisitiza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na sekta za umma na binafsi kuwezesha shughuli za uwekezaji kwenye sekta ya utalii na kuimarisha mchango wake katika uchumi wa nchi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abasi, amepongeza mafanikio yaliyotokana na filamu ya Royal Tour, akisema kuwa hii ni historia kwa Tanzania kushinda tuzo nyingi kwa mara moja.
Anasema baadhi ya wananchi walipinga matumizi ya fedha kwa filamu hiyo, wakitaka zielekezwe katika ujenzi wa madarasa, lakini sasa faida zake zimeanza kuonekana kwa vitendo. Dkt. Abasi ananukuu kauli ya Rais Dkt. Samia aliposema, "ipo siku Watanzania wataona manufaa ya filamu ya Royal Tour," na sasa ni dhahiri kwamba mafanikio hayo yanaonekana.
Katika kuhamasisha utalii wa ndani, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ameungana na wanawake wa Samia kutoka Mkoa wa Dodoma kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa utalii wa ndani.
Mkoa wa Dodoma umebarikiwa na vivutio vya kipekee ikiwemo mashamba ya zabibu, utamaduni wa wenyeji, na misitu ya asili. Wanawake wa Samia Mkoa wa Dodoma wamejikita kuhamasisha utalii wa ndani kwa kutembelea vivutio kama Pori la Swagaswaga na michoro ya mapango Kondoa.
Fatuma Madidi, Mwenyekiti wa Wanawake wa Samia Mkoa wa Dodoma, anasema, "Tunaunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhamasisha utalii wa ndani na kujivunia rasilimali za kipekee tulizonazo hapa nchini."
Hata hivyo Filamu ya Royal Tour imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuitangaza Tanzania kimataifa na kuongeza mwamko wa utalii wa ndani.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha uongozi wa kipekee katika kuonyesha uzuri wa nchi yetu, na faida zake zimeonekana kwa kuongezeka kwa idadi ya watalii, uwekezaji katika sekta ya utalii, na ajira kwa wananchi.
Sasa ni wakati wa Watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi hizi kwa kujivunia na kutembelea vivutio vyao vya ndani ili kuimarisha zaidi sekta hii muhimu kwa uchumi wa taifa.
0 Comments