Header Ads Widget

WAZIRI DKT JAFO AWATAKA WAKULIMA KUACHA KUCHANGANYA MAZAO.

 



NA MATUKIO DAIMA APP 

LINDI 

.Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt Seleman Jafo (mb) amewasisitiza wakulima kuhifadhi mazao yao katika mfumo wa stakabadhi za ghala yakiwa na ubora na kuacha tabia ya kuchanganya mazao hayo na mazao mengine au mchanga hali inayosababisha mazao hayo kushindwa kuuzika katika soko la kimataifa na kuchafua taswira ya nchi ya Tanzania ambayo imeingia mikataba ya biashara baina ya nchi Jumuiya za Kikanda na Kimataifa.

Waziri Jafo, ameyasema hayo Septemba alipokagua na kuweka Jiwe la Msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuongea na Wananchi wakati wa ziara maalum katika Wilaya ya Ruangwa ,Mkoani Lindi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiongozwa na kauli mbiu isemayo "Rais Samia na Maendeleo Wasikie na Waone" iliyoanza tarehe 17 - 21/09/2024 Mkoani Lindi.

Pia, Waziri Jafo ametoa rai kwa Wasimamizi wa Maghala kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kutoa huduma kwa uadilifu na uaminifu ili kuhakikisha mazao ya wakulima yanayohifadhiwa katika maghala hayo yanaingia na kutoka yakiwa na ujazo unaolingana ili kuvutia wafanyabiashara wa ndani na nje kutumia Mfumo huo.



Vilevile, Waziri Jafo ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo wilayani humo ambapo katika ziara yake amekagua ujenzi wa Mradi wa Usambazaji Maji unaujumisha Vijiji 56 vya Wilaya ya Ruangwa, Lindi na Nachingwea kutoka chanzo cha mto Nyangao (wilaya ya Lindi) na Ujenzi wa Barabara ya Mipingo yenye urefu wa Km. 0.78, Chuo cha Ufundi Stadi VETA, na kuzindua Mradi wa Jengo la ghorofa lenye madarasa 8, ofisi 4 na matundu 24 ya vyoo katika Shule ya Msingi Likangara.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Mhe. Hassan ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo Wilayani humo na kuahidi kuwa Wilaya yake itasimamia itekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa na kuhakikisha Miradi yote ya Maendeleo Wilayani humo inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi katika muda uliopangwa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI