Header Ads Widget

UJENZI WA BARABARA YA IRINGA -MSEMBE "BARABARA NI MAENDELEO NA MAENDELEO NI BARABARA"

 


Waziri wa ujenzi Innocent Bashungwa akizungumza na wananchi wa Iringa katika eneo la Mlandege mjini Iringa juzi wakati wa Hafla ya utiaji Saini mkataba wa ujenzi wa Barabara ya lami kati ya Iringa -Msembe yenye Kilimita 104 itakayojengwa kwa zaidi ya TSH 142.56 picha na Matukio Daima App 

NA MATUKIO DAIMA APP,

MAENDELEO ni barabara na  barabara ni maendeleo kwani huwezi kuzungumzia maendeleo bila uwepo wa Miundo mbinu Bora ya barabara na huwezi kutenanisha barabara na maendeleo yoyote yale .


Ifahamike kuwa barabara ni sehemu muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa taifa lolote Duniani .

Kwa  Nchini Tanzania, ujenzi wa barabara za kiwango cha lami umekuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi. 


 Katika hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa barabara hiyo iliyofanyika tarehe 21 Septemba 2024, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dkt. Pindi Chana, alisisitiza kuwa barabara hiyo itachangia kukuza utalii, hususan katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Sekta ya utalii ni mojawapo ya sekta muhimu inayochangia uchumi wa Tanzania kwa kutoa ajira na kuongeza pato la taifa. Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni moja ya hifadhi kubwa na maarufu zaidi nchini, inayovutia watalii wa ndani na wa nje kutokana na wingi wa wanyamapori na mandhari ya kuvutia. 

Hata hivyo, changamoto kubwa inayowakabili watalii wengi wanaotaka kutembelea hifadhi hii ni miundombinu duni ya barabara, hasa nyakati za mvua ambapo barabara nyingi huwa hazipitiki.

Kwa kujengwa kwa barabara ya lami ya Iringa-Msembe, itakuwa rahisi zaidi kwa watalii kufika katika Hifadhi ya Ruaha bila usumbufu wa barabara mbovu. 

Hii itasaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo, hasa kutoka nje ya nchi, na hivyo kuchochea ongezeko la mapato ya hifadhi na nchi kwa ujumla.

 Aidha, watalii wa ndani nao watafaidika kwa kuwa gharama za usafiri zitapungua, hali itakayowezesha Watanzania wengi zaidi kutembelea hifadhi hiyo na kujionea utajiri wa maliasili uliopo nchini.

Mbali na utalii, ujenzi wa barabara hii utatoa fursa nyingi za kiuchumi kwa wakazi wa Iringa na maeneo ya jirani. 

Galusi Msekwa ni mmoja kati ya wakulima wakubwa wilaya ya Iringa Vijijini anasema Barabara hii itachangia sana kuboresha usafirishaji wa mazao ya kilimo, hasa kutoka kwa wakulima wadogo wadogo ambao sasa wataweza kufikisha mazao yao sokoni kwa urahisi zaidi. 

Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa mkoa wa Iringa, na barabara hii itasaidia kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo kama mahindi, viazi, mboga, na matunda.

"Mimi nalima sana Nyanya sasa kama barabara hii itafunguka tunaweza ongeza Thamani ya Nyanya kwa kupeleka kuuza hifadhini na hata kuwauzia watalii"

Ujenzi wa barabara ya Iringa-Msembe utaleta manufaa makubwa kwa wananchi wa maeneo ya jirani, hususan katika sekta ya afya, elimu, na huduma nyingine za kijamii. Kwa sasa, wakazi wengi wa vijiji vinavyopitiwa na barabara hiyo wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kufikia huduma muhimu kutokana na hali mbaya ya barabara, hasa nyakati za mvua.

Rosemary Nyalusi ni mkazi wa Nzihi Moja kati ya vijiji vitakavyopitiwa na barabara hiyo anasema Kwao wanaipongeza serikali kwa kuanza ujenzi huo wa lami kwani Kwa upande wa afya, barabara ya lami itawarahisishia wananchi kufika katika hospitali na vituo vya afya vilivyopo mjini Iringa na maeneo mengine. 

Hii itasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, hasa kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka kama wagonjwa wa ajali au kina mama wajawazito. 

Nyalusi anasema   ujenzi wa barabara hii utaboresha usambazaji wa dawa na vifaa tiba katika zahanati na vituo vya afya vya vijijini, hali itakayochangia kuboresha utoaji wa huduma za afya katika maeneo ya ndani.

Pius Ndelwa na Stanislaus Mhongole  kati ya Walimu wastaafu mkoani Iringa wanasema  Kwa upande wa elimu, barabara ya Iringa-Msembe itakuwa na mchango mkubwa katika kuongeza mahudhurio ya wanafunzi mashuleni, hasa wale wanaosafiri kutoka maeneo ya mbali. 

Barabara hiyo itawarahisishia wanafunzi kufika shuleni kwa wakati na kwa usalama zaidi, hali itakayosaidia kuboresha kiwango cha elimu katika maeneo ya vijijini.

Kwa upande wa walimu na wafanyakazi wa elimu watapata urahisi wa kusafiri kwenda na kutoka shule, hivyo kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu.


George Kaundama ni mmoja kati ya wamiliki wa Hotel mjini Iringa anasema Ujenzi wa barabara ya lami ya Iringa-Msembe utaleta fursa nyingi za uwekezaji, hasa katika sekta ya utalii na huduma za kijamii. 

Wawekezaji wa ndani na wa kimataifa wanaweza kuanzisha miradi ya kibiashara kama hoteli, migahawa, vituo vya mafuta, na vituo vya huduma za kijamii kando ya barabara hiyo. 

Hifadhi ya Ruaha, kama ilivyo kwa vivutio vingine vya utalii nchini, inahitaji uwepo wa huduma bora za malazi kwa watalii, na ujenzi wa barabara hii utaleta fursa kubwa kwa wawekezaji kuanzisha hoteli na kambi za watalii karibu na hifadhi hiyo.

Pia, ujenzi wa barabara hii utafungua fursa za uwekezaji katika sekta ya kilimo. Wakulima wa Iringa watapata urahisi wa kusafirisha mazao yao hadi sokoni, hali itakayowezesha kuanzishwa kwa viwanda vidogo vya kuchakata mazao ya kilimo kama viazi na mboga. 

Vilevile, usafirishaji wa mazao ya misitu kama mbao na asali kutoka maeneo ya vijijini hadi masoko ya mijini utakuwa rahisi zaidi, hali itakayochangia kuongeza mapato kwa wakulima na serikali kwa ujumla.


Said Omari ni mmoja kati ya Watoa huduma za usafiri kati ya Iringa -Msembe anasema Barabara ya lami ya Iringa-Msembe pia itakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya usafirishaji katika mkoa wa Iringa na maeneo ya jirani. 

Kwa sasa, magari mengi yanayopita katika barabara hiyo yanakabiliwa na changamoto za ubovu wa barabara, hali inayosababisha ucheleweshaji wa mizigo na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji. 

Kwa kujengwa kwa barabara ya lami, usafirishaji wa bidhaa na abiria utaimarika, hali itakayochangia kupunguza gharama za usafiri na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi.

Aidha, barabara hii itarahisisha usafirishaji wa watalii kutoka maeneo mengine ya Tanzania hadi Hifadhi ya Ruaha. 

Michael Sanga ni mmoja wa watalii wa ndani kutoka mkoa wa Iringa anasema kupitia barabara hiyo Watalii wanaotoka katika mikoa ya jirani kama Mbeya, Njombe, na Dodoma wataweza kufika hifadhini kwa urahisi zaidi kupitia barabara hii, hali itakayochangia kuongeza idadi ya watalii na mapato yanayotokana na utalii katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Mbunge wa Jimbo la Ismani Wiliam Vangimembe Lukuvi ambae pia ni Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera na uratibu wa bunge anasema wananchi wake wamesuburi kwa hamu kubwa ujenzi wa Barabara hiyo na hata Leo wanaposhuhudia hafla ya kusainiana mkataba kati ya mkandarasi na serikali Furaha Yao imeongezeka .

Lukuvi anampongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ndoto za wananchi wake na kuwa ahadi ya ujenzi wa Barabara hiyo ilikuwepo muda mrefu na awamu zaidi ya Mbili ziliahidi ujenzi wa Barabara hiyo ila ni awamu hii ya sita chini ya Rais Dkt Samia ahadi inakwenda kutekelezwa.

Pamoja na mbunge Lukuvi pia mbunge wa Kalenga Jackson Kiswaga na mbunge wa Jimbo la Iringa mjini Jesca Msambatavangu wanaipongeza serikali kwa ujenzi huo kuanza na kuwa kwa majimbo yao uchumi wa wananchi wao utapata zaidi.


Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (Mb) amesema Barabara hiyo pamoja na mambo mengine itatoa mchango mkubwa katika shughuli za utalii kwenye Hifadhi ya Taifa Ruaha iliyopo Mkoani Iringa.

"Utalii ili uweze kustawi lazima miundombinu iwepo hivyo barabara hii itakuza utalii ikiwa ni  fedha ambazo  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha kujengwa kwa Barabara hii" amesema.

Kumbuka  miradi mikubwa inayokusudiwa kutekelezwa kwa sasa ni ujenzi wa barabara ya lami kutoka Iringa hadi Msembe, yenye urefu wa kilomita 104 barabara hii imesubiriwa kwa muda mrefu na hata sasa kuanza kwake bado imechelewa sana ila kuchelewa kwake ni mchakato wa kawaida kwenye maendeleo yoyote yale.

 Barabara hii inatarajiwa kugharimu takriban shilingi bilioni 142.56 na itakuwa kiunganishi muhimu kati ya mkoa wa Iringa na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha hivyo kufungua kwa Kasi kubwa Utalii wa kusini na kukuza Pato la mtu mmoja mmoja wa mkoa wa Iringa na Pato la Taifa pia.

Ujenzi wa barabara ya Iringa-Msembe ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuboresha miundombinu ili kufungua fursa za kiuchumi, hasa katika sekta ya utalii, kilimo, na huduma za kijamii.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Wabunge wa Mkoa wa Iringa, Viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, Watendaji na Watumishi wa Taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na wananchi wa Mkoa wa Iringa

Akizungumza kwa niaba ya Chama Cha mapinduzi (CCM)mkoa wa Iringa juu ya ujenzi huo mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa NEC Salim Abri Asas aliipongeza serikali kwa ujenzi wa Barabara hiyo kuwa ujenzi huo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa vitendo .

Alisema ujenzi wa barabara ya lami ya Iringa-Msembe ni mradi wa kimkakati unaotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika uchumi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Taifa kwa ujumla. 

"Barabara hii itafungua milango ya fursa nyingi za kiuchumi, hasa katika sekta ya utalii, kilimo, na huduma za kijamii "

Pia alisema barabara hii itachangia kuimarisha sekta ya usafirishaji na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuanzisha miradi ya kibiashara kando ya barabara hiyo.

Asas alisema Kwa kujengwa kwa barabara hii, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha itapata nafasi ya kuvutia watalii wengi zaidi, hali itakayosaidia kuongeza mapato ya hifadhi hiyo na serikali kwa ujumla. 

Hata hivyo alisema  wananchi wa Iringa na maeneo ya jirani watanufaika kwa kupata huduma bora za kijamii na fursa za kiuchumi zitakazotokana na uwepo wa miundombinu bora. 

Kuwa  ujenzi wa barabara hii ni hatua muhimu katika juhudi za serikali za kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi na kukuza uchumi wa Taifa.

Sera ya Taifa ya Ujenzi wa Barabara nchini Tanzania inalenga kuhakikisha kuwa miundombinu ya barabara inaboresha ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii.

 Sera hii inatoa miongozo ya kuboresha na kupanua mtandao wa barabara ili kurahisisha usafiri, kuunganisha maeneo ya mijini na vijijini, na kukuza biashara na uchumi.

Misingi ya sera hii ni Kuimarisha miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri wa watu na mizigo, Kuweka kipaumbele kwa maeneo ya kimkakati kama vile hifadhi za taifa, maeneo ya uzalishaji wa mazao, na viwanda ili kukuza uchumi wa nchi.


Pamoja na  Kuhakikisha usalama barabarani kwa kuboresha ubora wa barabara na kuweka alama sahihi,Kuhamasisha ushirikiano wa sekta binafsi katika ujenzi na matengenezo ya barabara na  Kupunguza gharama za usafiri na kupunguza muda wa kusafiri kwa kuongeza mtandao wa barabara bora na salama.

Hivyo ni ukweli usiopingika kuwa Sera ya Ujenzi wa Barabara inalenga kuimarisha ukuaji wa uchumi kwa kuunganisha maeneo mbalimbali na kuwezesha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa ufanisi zaidi ndio maana tunasema Maendeleo ni Barabara na barabara ni maendeleo.

Makala haya imeandikwa na Francis Godwin ambae ni mtayarishaji wa maudhui katika mtandao wa Matukio Daima media anapatikana kwa namba 0754026299



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI