1. Uwepo wa Matumizi Mabaya ya ARV's katika Ufugaji
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imepokea taarifa kuhusu baadhi ya wafugaji wanaotumia dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI (ARV's) kwa njia isiyofaa, kwa lengo la kunenepesha mifugo yao. Matumizi haya yanakiuka sheria na yanahatarisha afya ya jamii.
2. Madhara ya Matumizi Haya kwa Afya ya Jamii
TMDA inatoa onyo kali kwa wafugaji wote wanaojihusisha na matumizi haya yasiyofaa ya ARV's. Dawa hizi zimetengenezwa maalum kwa ajili ya kupunguza makali ya virusi vya UKIMWI kwa binadamu baada ya mgonjwa kushauriwa na daktari. Matumizi ya dawa hizi kwa mifugo yanaweza kusababisha athari mbaya kwa afya ya binadamu, kutokana na kuingia kwa mabaki ya dawa kwenye mnyororo wa chakula.
3. Uchunguzi na Hatua za Kisheria
TMDA inawataka wafugaji wanaotumia ARV's kwa mifugo kuacha mara moja. Mamlaka imeanzisha uchunguzi wa kina katika mashamba mbalimbali ya mifugo ili kubaini wanaohusika na vitendo hivi. Mtu yeyote atakayebainika kutumia dawa hizi kwa njia isiyofaa atachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kuharibiwa kwa mifugo ambayo itabainika kuwa si salama tena kwa matumizi ya binadamu.
4. Wito kwa Wananchi Kutoa Taarifa
TMDA inatoa wito kwa wananchi kushirikiana na mamlaka katika kutoa taarifa endapo watashuhudia au kushuku matumizi hayo hatari ya ARV's katika mifugo.
Taarifa zinaweza kutolewa kupitia ofisi za TMDA Makao Makuu, ofisi za kanda zilizopo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma, Songea, Tabora, na Geita.
Aidha, taarifa zinaweza kutumwa kupitia barua pepe info@tmda.go.tz au kwa kupiga simu bila malipo kupitia namba 0800110084.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)
Kiwanja Na. 56/1, Barabara ya Hombolo,
Mkabala na Shule za Martin Luther,
S.L.P 1253, Dodoma
Simu bila Malipo
0 Comments