Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA
MIFUKO na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi zaidi ya 20 inatarajia kushiriki maonyesho ya saba ya kitaifa ya mifuko hiyo yanayofanyika kuanzia Septemba 8 hadi 14 mwaka huu mjini Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, akizungumza jana alisema maonyesho hayo yatafunguliwa Septemba 10, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu,William Lukuvi na yatafungwa na Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa.
Alisema Mkoa wa Singida umejiandaa kikamilifu kuwa mwenyeji wa maonyesho ambapo maandalizi yote muhimu yamekamilika ili kuhakikisha wageni kutoka mikoa mbalimbali wanapokelewa na kuhudumiwa vizuri.
Dendego alisema lengo la maonyesho hayo ni kuwaletea wananchi wa Mkoa wa Singida na mikoa jirani na Watanzania kwa ujumla taarifa sahihi za mifuko hiyo ya uwezeshaji na programu zake ili waweze kunufaika nazo.
Alisema wafanyabiashara wa mkoa wa Singida watumie fursa ya maonyesho hayo kuuza bidhaa zao na kutoa huduma nzuri na kuepuka upandishaji wa bei usioeleweka ili wageni watamani kurudi tena Singida.
"Nitumie fursa hii kuwaomba wananchi wa Mkoa wa Singida kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuhudhuria maonyesho haya ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji," alisema.
Alisema maonesho haya yanatoa nafasi ya pekee kwa wananchi kupata uelewa wa kina kuhusu programu mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi na jinsi wanavyoweza kunufaika nazo
Dendego akizungumzia hali ya ulinzi na usalama alisema, serikali ya mkoa imejipanga kikamilifu ili kuhakikisha usalama wa wageni na washiriki wote wa maonesho hayo lengo likiwa ni kuboresha nafasi ya Singida kama kituo cha mikutano na maonesho.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), BmBeng’i Issa, alisema kuwa maonesho hayo yatakuwa na taasisi nyingi zinazotoa mikopo na ruzuku kwa ajili ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
"Tuna matarajio makubwa ya watu kushiriki vizuri na kupata huduma na fursa mbalimbali kupitia programu mbalimbali na mifuko ya uwezeshaji hapa nchini. Hii itatusaidia kuinua uchumi wetu binafsi," alisema.
0 Comments