NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Vunjo lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro Dkt Charles Stephen Kimei ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha shilingi bilioni 3.681 za kujenga barabara ya kiwango cha kisasa kutoka Himo - Makuyuni - Lotima hadi mpakani mwa Wilaya ya Mwanga na Moshi.
Ujenzi wa barabara hiyo utafanywa na Mkandarasi Kampuni ya Kings Builders Limited ya kitanzania ambayo imepewa zabuni ya kujenga barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 6.115 kwa muda wa miezi sita toka sasa ambapo kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa barabara, mitaro, madaraja, vivuko maeneo ya makazi ya wananchi na uwekaji wa taa.
Kimei ametoa shukrani hizo wakati wa makabidhiano ya barabara hiyo kwa mkandarasi ulliosimamiwa na Mratibu wa TARURA Mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Nicolas Francis eneo la soko la Himo, kata ya Makuyuni ambapo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Ummy Nderiananga alikuwa mgeni rasmi.
Dkt Kimei amesema kilio chao kikubwa cha wananachi kilikuwa ni kujengwa kisasa ambapo kwa sasa kimepatiwa majawabu kwa serikali ambapo tayari imetoa fedha na mkandarasi amekabidhiwa mradi kwa ajili ya ujenzi huo.
Ameendelea kwa kusema barabara hiyo ni barabara ya kimkakati ambayo itarahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria, mazao ya kilimo, kuchagiza shughuli za kibiashara pamoja na wananchi kufuata huduma za kijamii kama elimu na afya katika mji wa Himo.
Aidha aliongeza barabara hiyo itatumika kama by pass ya magari na hivyo kuipunguzia foleni barabara kubwa inayotoka Dar es Salaam kupita Njiapanda.
Naye Katibu wa CCM wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Mahanyu alisema ujenzi wa barabara hiyo ni matokeo ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM na mwendelezo wa utamaduni wa chama hicho wa kuahidi na kutekeleza na kuwataka wananchi wa kata hiyo waendelee kujenga imani na chama hicho ili waendelee kunufaika na maendeleo.
Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Makuyuni wameishukuru serikali na kumpongeza Mbunge Kimei kwa kuweza kufanikisha kuanza kwa ujenzi wa barabara hiyo ambayo imesubiriwa kwa miaka 25 na itaharakisha maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi hasa usafirishaji wa uhakika wa abiria na mazao ya kilimo.
Walisema kukamilika kwa ujenzi wake kutapunguza gharama za usafiri na usafirishaji wa abiria na mazao ya kilimo hayo kwenda kwenye masoko ya Himo, Marangu, Mwika, Moshi Mjini, Rombo, Mwanga na Nchi jirani ya Kenya hali itakayoongeza thamani ya mazao ya wakulima na kuchochea hali ya biashara tofauti na sasa kutokana na kuwepo changamoto ya ubovu wa barabara hiyo.
Mwisho.
0 Comments