Na, Matukio daima App,
Hukumu ya kesi ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti, mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam inayowakabili washtakiwa wanne wakiwamo askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wa Magereza, itatolewa leo Jumatatu, Septemba 30, 2024.
Kesi hiyo ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024 inawakabili washtakiwa wanne akiwamo MT 140105 Clinton Damas, maarufu Nyundo ambaye ni askari wa JWTZ, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.
Ijumaa ya Septemba 27, 2024, wakili wa washtakiwa hao, Meshack Ngamando akizungumza na waandishi wa habari alisema kila kitu kilichotakiwa kwenye kesi hiyo kilikuwa kimekamilika, hivyo kinachosubiriwa ni uamuzi wa Mahakama.
Alisema siku hiyo ya Ijumaa walifanya mawasilisho ya mwisho ya kisheria kuhusu mwenendo mzima wa kesi hiyo na kwamba wamewasilisha hoja kuhusu kasoro zilizojitokeza wakati wa usikilizwaji.
"Tumepata nafasi ya kuwasilisha mawasilisho ya mwisho, kuhusu mwenendo wote wa kesi kuanzia hati ya mashtaka, ukamataji, utambuzi, mashahidi, vielelezo vilivyotolewa mahakamani kwa muda wa saa tatu kuanzia saa nane mchana hadi saa 11.00 jioni.
“Upande wa Jamhuri pia umewasilisha yao kuanzia saa 11.00 jioni hadi saa moja usiku, kwa hiyo kinachosubiriwa kwa sasa ni uamuzi wa Mahakama," alisema Ngamando.
0 Comments