Header Ads Widget

GWAMAKA MBUGHI AJITOSA UBUNGE ILEJE 2025, CHADEMA WAFUNGUKA.

 






NA JOSEA SINKALA, SONGWE.

Aliyekuwa Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyasa Gwamaka Mbughi, ametangaza nia ya kugombea ubunge kwa tiketi ya Chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani 2025 ili kumwondoa Naibu Waziri wa ujenzi Godfrey Kasekenya Kasongwa ambaye ndiye mbunge wa sasa wa jimbo la Ileje kama atagombea tena.


Gwamaka Mbughi ametoa tangazo hilo kwa umma kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Ikumbilo kata ya Chitete Ileje mkoani Songwe akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Chama na mabaraza mikoa mbalimbali ya kanda ya Nyasa.


Amesema amedhamiria kugombea ubunge kwani amejipima anao uwezo na kuomba ushiriki wa wananchi kuhakikisha wanapata wawakilishi sahihi.


"Ndugu zangu wa Ileje katika hatua ya sasa sitazungumza kuhusu bei za mazao yetu ya Ileje, sitazungumza kuhusu umasikini uliopo Ileje badala yake nimekuja kwa agenda moja tu nayo ni kupata baraka zenu kwenye safari ambayo nimeichagua. Kwa maana hiyo mimi nimetia nia ya mwakani kugombea ubunge jimbo la Ileje kwasababu nimejipima na ninaweza kuwa mbunge wenu", ameeleza Gwamaka Mbughi.


Kiongozi huyo mtendaji wa zamani wa CHADEMA kanda ya Nyasa, amesema anao uhakika wa kushinda na kuwawakilisha vema wananchi wa Ileje ambao pamoja na raslimali mbalimbali lakini bado wanakabiliwa na ufukara.


Kwa upande wake mgeni rasmi wa mkutano huo Makamu mwenyekiti wa CHADEMA kanda ya Nyasa Frank George Mwakajoka, amewataka wananchi kwenda kujiandikisha kwenye daftari la mkazi na kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi bora kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji kisha uchaguzi mkuu mwaka 2025.


Mwakajoka amekemea kuendelea kushamiri kwa vitendo vya utekaji, watu kupotea na mauaji ya wananchi akisema "Serikali imeona imeshindwa kuwaletea maendeleo sasa imeanza kuteka watu, mimi nilijua Serikali hii itakuwa angalau lakini imekuwa zaidi kwahiyo twende tukajiandikishe tuhakikishe tunachagua viongozi bora".


Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Songwe Isakwisa Thobias Lupembe, amesema katika chaguzi zijazo CHADEMA hasa katika mkoa wake haitaruhusu kuona mgombea wake yeyote anakatwa jina au kuwepo kwa viongozi wa kupita bila kupingwa.


Rose Mayemba ni mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Njombe, amewataka wananchi kubadili fikra zao na kwenda kufanya mabadiliko kuanzia Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji akisema ndio msingi wa uchaguzi mkuu mwaka 2025 kuhakikisha wanapata viongozi imara.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI