KUTOKANA na kuongezeka kwa matukio ya ukatili wa kijinsia nchini Taasisi ya Foundation For Disabilities Hope (FDH) imeanza kutekeleza mradi wa kuzuia vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto wenye ulemavu.
Akizungumza jana wilayani hapa, wakati wa mafunzo ya namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto wenye ulemavu Mratibu wa mradi wa chukua hatua sasa zuia ukatili, Glory Mbowe alisema lengo ni kuzunia vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto wenye ulemavu.
“Lakini pia malengo mahususi ni kutoa elimu juu ya masuala ya ukatili na haki za binadamu ili wanawake na watoto wenye ulemavu waweze kutambua haki zao za msingi lakini pia kuwajengea uwezo wanawake na watoto wenye ulemavu kuripoti vitendo vya ukatilii kwenye vyombo husika”alisisitiza Mbowe.
Aidha, alisema mradi huo ambao unatekelezwa katika wilaya ya Chamwino katika Kata ya Buigiri utatumika pia kutoa mafunzo ya namna gani watu wenye ulemavu wanaweza kukabiliana na vitendo vya ukatili.
“Mafunzo haya yatasaidia kuongeza uelewa kwa wanawake na watoto wenye ulemavu kuwa na uwezo wa kutambua haki zao za msingi na pale wanapofanyiwa ukatili ni hatua gani wachukue ili kuondokana na kadhia hiyo”alisema Mbowe
Mwezeshaji katika mafunzo hayo kutoka dawati la jinsia kituo cha polisi wilaya ya Chamwino Malale Michael, alisema moja kati ya vitu ambavyo wanawafundisha wanawake na watoto wenye ulemavu ni kujua maana ya ukatili.
“Tunawafundisha kwanza kujua ukatili ni nini lakini pia upo wa aina gani lakini wakisha jua nini ukatili wanawezaje kutoa taarifa za matukio ya ukatili ili vyombo husika viweze kuchukua hatua na kukomesha vitendo hivyo”alisema Malale.
Aidha, alisema wilaya ya Chamwino bado inakabiliwa na matukio ya ukatili ikiwemo ndoa za utotoni pamoja na ulawiti na ubakaji.
“Hali ya vitendo vya ukatili katika wilya hii siyo mbaya sana wala siyo nzuri sana lakini matuki haya bado yapo na sisi kama jeshi polisi tumeanzisha kampeni ya kuzuia hali hiyo inayosema tuchukue hatua kabla hawaja haribiwa”alisema.
Pia, alisema wamekuwa wakitoa elimu kutumia nyumba za ibada ili kuwapa uelewa wananchi kuhusu vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto wenye ulemavu.
Mwanasheria wa Taasisi ya FDH, Joyce Mhana alisema kwa mujibu wa Katiba ya nchi ya mwaka 1977 kila binadamu ni sawa hivyo hakuna sababu ya mtu kumfanyia ukatili wa aina yoyote.
“Lakini pia ipo sharia namba tisa ya mwaka 2010 ambayo inasema kuwa watu wenye ulemavu wanapaswa kulindwa na inatoa wajibu kwa watu wengine kumlinda na kwa yule ambaye ataoneka kushindwa kutimiza na yeye atachukuliwa kama ni sehemu ya wanaofanya ukatili huo”alisema.
0 Comments