NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Mbeya Masaga Pius Kaloli, amesema CHADEMA haitakubali viongozi wa kupita bila kupingwa katika chaguzi zijazo za Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Amesema hayo wakati akizungumza na wajumbe wa baraza la mashauriano mkoa wa Mbeya alipoongoza kikao hicho cha kwanza tangu wachaguliwe.
"Sasa kuna mambo ambayo Chama cha Mapinduzi na Serikali wanaendelea kuwafanya ambayo kimsingi yamekuwa ni tishio kubwa sana kwa wananchi kutokuwa na imani na uchaguzi huu wa Serikali za mitaa na mambo hayo nikama mambo ya utekaji yanayoendelea nimkakati muhimu sana wa Serikali ya CCM ambao tunaamini lengo lao ni kuwatia wa-Tanzania hofu waogope kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa, waogope kuendelea kupigania haki zao na mnakumbuka hata mkoa wa Mbeya kuna kijana aliyetekwa mpaka leo haonekani alipo", ameeleza mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Mbeya Masaga Kaloli.
Mwenyekiti huyo amesema kauli zinazoendelea kutolewa na baadhi ya viongozi wa Serikali akiwemo aliyekuwa Waziri wa Habari Nape Nnauye kuwa matokeo yanategemea mtu anayehesabu na kutangaza kura pamoja na ile ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido kuwa madiwani wa Wilaya hiyo walipita bila kupingwa mwaka 2020 ni Mungu anaendelea kuwaumbua.
Pamoja na mengi aliyoyaongea amewataka wana-Chadema na wananchi kwa ujumla kuendelea kujiandaa na chaguzi hizo hasa uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa kuhakikisha wakati utakapowadia wajiandikishe na kujitokeza kuchagua viongozi bora na kulinda kura.
Katika kikao hicho wamezindua mpango kabambe wa K3 yaani Kujiandikisha, kuchagua na kulinda kura wakati ukifika.
"Na leo (Sept.02, 2024) tunatangaza operesheni yetu ambayo tutakwenda nayo ya K3 ambayo ni Kujiandikisha, kupiga kura na kulinda kura, tutatembea nayo kwenye majimbo, vijiji vyote vya mkoa wa Mbeya kuhakikisha tunatoa elimu sahihi maana tumeona tume ambayo ni TAMISEMI haina nia njema", amesema mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Mbeya Masaga Kaloli na kuongeza;
"Kwasababu Demokrasia inakanyagwa ndani ya Taifa letu wenyewe hatutakubali mara hii, hatutakuwa wazembe, uchaguzi huu sisi tumeuchukulia ni au tuendelee kuishi au wote tufe ili watawale wenyewe wakitutawala pamoja na makaburi yetu na sisi hatutakuwa watu wa kwanza kufa kwa ajili ya kupigania haki, sisi tunataka uchaguzi ulio huru na wa haki. TAMISEMI kuendelea kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa ikiwa ni mikakati yake ya kuendelea kutuibia uchaguzi sisi CHADEMA hasa mkoa wa Mbeya hatutakubali", amesisitiza mwenyekiti Masaga.
Naye mwenyekiti wa Baraza la wazee wa CHADEMA (BAZECHA) mkoa wa Mbeya John David Mwambigija amewataka wazee wote katika mkoa huo, viongozi wa Chama na mabaraza na wanachama kwa ujumla kuendelea kushikamana ili kuhakikisha CHADEMA inashinda uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Baraza la vijana (BAVICHA) mkoa wa Mbeya Evaristo Elisha Chonya amewataka vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kwenda kuwa sehemu ya maamuzi na kuwa na hatma bora ya Taifa lao kuanzia Serikali za mitaa hadi uchaguzi mkuu na kusisitiza kulinda kura kipindi cha chaguzi.
"Niwasisitize tu vijana wote hasa mkoa wa Mbeya tujitokeze kugombea nafasi mbalimbali, lakini pia tukalinde kura tukishapiga kura hatutamwachia askari zile kura ni zetu, ni mali yetu kwahiyo tukipiga kura tukahakikishe tunalinda kura", amesema Chonya.
Hiki ni kikao cha kwanza cha Baraza la mashauriano mkoa wa Mbeya tangu kuchaguliwa kwa uongozi mpya wa CHADEMA mkoa wa Mbeya ambapo baraza hili la uongozi linakabiliwa na masuala ya uchaguzi wa Serikali za mitaa vitongoji na vijiji baadaye Novemba mwaka huu ikiwa ni majirio ya uchaguzi mkuu wa mwakani 2025 pamoja na mikakati mbalimbali ya kuendelea kukijenga chama hicho kikuu cha upinzani Tanzania hasa upande wa bara.
0 Comments