Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewalika wananchi kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Singida kujitokeza kwa wingi kupata huduma zinazotolewa na wakala huo kwenye maonesho ya saba ya kitaifa ya Mifuko ya Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yanayofanyika viwanja vya Bombadia mjini Singida.
Afisa Leseni Mwandamizi kutoka BRELA, Rehema Kionaumela, ametoa wito huo leo (Septemba 10, 2024) wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho hayo.
"Watu wote ambao hawajui BRELA inafanya nini wakija kwenye banda letu watajifunza na kuhudumiwa papo kwa papo, wakija mfano wenye viwanda vidogo tunaweza tukawasajili hapa ,pia kwa wafanyabiasha wale wanaosafirisha biashara zao au wale wanaofanya biashara nje ya nchi waje tuwajisajili," amesema.
Kionaumela amesema katika usajili kwa upande wa biashara mwananchi yeyote ambaye anafanya biashara hata kama hana au anategemea kufanya biashara anatakiwa kuwa na namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA),namba ya simu pamoja na email anaweza kupata jina la biashara papo hapo.
Amesema manufaa ya kusajiliwa ni kubwa mfano kwa anayetaka kusajili biashara kwani biashara yake itajulikana na anaweza kupata mkopo benki na taasisi nyingi zinaweza kumpa pesa na kujenga uaminifu kwa wateja wake.
Majukumu ya BRELA ni pamoja na kusajili Makampuni, Majina ya Biashara, Alama za Biashara na Huduma, Viwanda vidogo, kutoa Hataza, Leseni za Biashara kundi A na Leseni za Viwanda.
BRELA pia imeboresha utoaji wa huduma kwa kutumia mifumo ya usajili kwa njia ya mtandao kupitia Online Registration System (ORS) na utoaji wa Leseni za Biashara kupitia Tanzania National Business Portal (TNBP).
MWISHO
0 Comments