Header Ads Widget

WANANCHI WACHANGA MILIONI 6.5 KUJENGA MRADI WA MAJI LUSITU NJOMBE

 



Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE

Wananchi wa kijiji cha Lusitu kata ya Luponde Halmashauri ya mji wa Njombe mkoani Njombe wamelazimika kuchangishana zaidi ya shilingi milioni 6.5 ili kujenga mradi wa maji utakaowasaidia kuepukana na adha ya kufuata maji mabondeni hadi majira ya usiku.


Hatua hiyo imekuja kufuatia kukosa maji ya bomba kwa miaka mingi ilihali vijiji vingine vya kata ya Luponde vikiwa na maji jambo lililowasukuma kuchukua jitihada binafsi badala ya kuendelea kuisubiri serikali iwasaidie.



Kutokana na Jitihada za wakazi hao Serikali ya wilaya ya Njombe chini ya Mkuu wake wa Wilaya Kissa Gwakisa Kasongwa na kamati yake ya Ulinzi na Usalama ikalazimika kufika na kuwaunga mkono kwa kuchangia zaidi ya shilingi milioni moja huku akiagiza Wakala wa Maji vijijini Ruwasa kuhakikisha wanasaidia kupatikana kwa maji hayo ndani ya wiki tatu.


Mtaalamu wa Maji toka RUWASA Wilaya ya Njombe Bakari Kitogota anakiri kupokea maelekezo ya serikali na kuahidi kutoa fedha zote za kukamilisha mradi huo.


Awali Diwani wa kata ya Luponde Yurick Msemwa amesema adha ya ukosefu wa maji kwa wakazi wake iliwapa hasira na kuamua kuacha kusubiri serikali iwapelekee maji.


Baadhi ya wananchi wa Lusitu akiwemo Produse Kilumile na Salima Msigwa wameonesha furaha yao baada ya serikali ya wilaya kufika na kuwachangia fedha za kukamilisha mradi huo na kwamba sasa adha kwa akina mama zitapungua Endapo mradi utakamilika.



Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini Deo Mwanyika aliyechangia shilingi Milioni moja katika ujenzi wa mradi huo kupitia katibu wake Andreas Mahali ametuma ujumbe wa kulinda mradi huo utakapokamilika.


Changamoto ya ukosefu wa maji kwa wananchi hususani vijijini imekuwa kero kubwa katika maeneo mengi hapa nchini na kusababisha baadhi ya ndoa kuvunjika kutokana na muda mwingi kutumika kutafuta maji umbali mrefu.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI