Header Ads Widget

SHUGHULI ZA UVUVI ZAANZA RASMI ZIWA TANGANYIKA

 

 

Waziri wa mifugo na uvuvi Abdallah Ulega (katikati) akikata utepe kuzindua rasmi shughuli za uvuvi katika ziwa Tanganyika baada ya kupumzishwa kwa miezi mitatu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akimkabidhi Kasha la kuhifadhia samaki mmoja wa Kinamama, anayejishughulisha na shughuli za uvuvi katika Mwalo wa Katonga  Ziwa Tanganyika. Tukio hilo limefanyika mkoani Kigoma katika Mwalo wa Katonga muda mfupi baada ya Waziri huyo kutangaza kufunguliwa kwa ziwa hilo  Agosti 15, 2024.

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amezindua zoezi la uvuvi katika  Ziwa Tanganyika baada ya kupumzishwa kwa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo  kwa miezi mitatu.

Waziri Ulega amezindua zoezi hilo katika Mwalo wa Katonga manispaa ya Kihoma Ujiji  mkoani Kigoma Agosti 15 na kubainisha kuwa kupumzishwa kwa shughuli za uvuvi kwa miezi mitatu kuanzia Mei 15 hadi Agosti 15 mwaka huu kulikuwa kunalenga kulinda rasilimali za uvuvi kwenye ziwa hilo.

Amesema uamuzi huo wa kupumzisha ziwa ni utekelezaji wa Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA) Unaoweka Hatua za Usimamizi wa Uvuvi Endelevu katika Ziwa Tanganyika na Bonde lake. 


Waziri huyo wa mifugo na uvuvi alisema kuwa haitakuwa na maana serikali kutumia mitutu ya bunduki kuzuia watu wasivue wakati wa kupumzishwa kwa ziwa wala haina nia ya  kuwakomoa watu kwani jambo hilo la kupumzishwa shughuli za uvuvi linafanywa kwa manufaa ya Watanzania wote na linafanywa kwa kuwashirikisha wadau wote na wananchi wote.

 Aidha, Waziri Ulega ametumia  jukwaa hilo kuwaelekeza wavuvi kuwa kufunguliwa kwa shughuli za uvuvi kuendane na matumizi sahihi ya zana na njia halali zinazokubalika kisheria ili samaki walioachwa wazaliane na kukua waendelee kupatikana. 

Akizungumza katika zoezi hilo Naibu Katibu Mkuu wizara ya mifugo na Uvuvi, Dk.Edwin Mhede alisema kuwa uvuvi imekuwa moja ya sekta kuu ya uchumi nchini ikiajiri watanzania milioni sita  Sawa na asilimia 10 ya Watanzania wote.

Mmoja wa wananchi waliohudhuria ufunguzi huo Songoro Athumani anayemiliki mitumbwi ya uvuvi  kutoka kijiji cha Kalilani  wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma alisema wanaunga mkono mpango huo wa serikali wa kupumzisha shughuli za uvuvi kwa muda  kwani umesaidia kuongeza mazao ya uvuvi kutokana na samaki na dagaa kuonekana kwa wingi hata kabla uvuvi haujaanza.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI