Na Gabriel Kilamlya Matukio DimaAPP NJOMBE
Wakati Wizara ya Afya ikiendelea kutekeleza kampeni ya Mtu ni Afya chini ya Kaulimbiu ya Fanya kweli Usibaki Nyuma,Halmashauri ya wilaya ya Njombe wamesema mkazo mkubwa kwao ni kwa upande wa Afua za Mazoea na Lishe bora kwani katika Usafi wa mazingira na Vyoo bora wao wamekuwa mfano mzuri katika Taifa.
Hayo yanajiri wakati timu ya Kampeni hiyo ikiongozwa na Mhamasishaji Mkuu msaani wa Mashairi Mrisho Mpoto[Mjomba] ilipofika katika kijiji cha Havanga Kata ya Kidegembye na Kata ya Matembwe imeelezwa kuwa hatua ya sasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ni kuegemea kwenye Afua nyingine na sio ya Usafi wa Mazingira na Vyoo bora kwani huko wamefanikiwa pakubwa.
Ofisa Afya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Evelyne Kidenya anasema hatua hiyo itasaidia wananchi kuepukana na changamoto nyingine za kiafya kwani wakifanya mazoea na kupata mlo kamili itawasaidia kuboresha afya na kujenga miili yao.
Serikali ya Kijiji cha Havanga chini ya Mwenyekiti wake Athanas Mputa na Elphas Lulima Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho wamesema awali haikuwa rahisi kutekeleza kampeni hiyo lakini baada ya elimu na mahusiano mazuri na Wananchi wao walifanikisha kwa kiasi kikubwa hadi wanaibuka washindi kitaifa katika kampeni hiyo.
Apollo Kingililwe na Wema Madege ni wananchi wa Kijiji cha Havanga ambao wanasema kutekeleza vyema kampeni ya ujenzi wa vyoo bora na mazingira kuliwasaidia kuepukana na magonjwa ya mlipuko na sasa wanaishi kwa furaha na Amani.
Kwa upande wake Mganga mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Dokta Frank Mganga anasema wanahitaji kufanya kweli kwenye kufungua majadiliano upande wa Hedhi Salama ambako mambo yanafanyika kwa usiri mkubwa ilihali ni jambo la kawaida katika maisha ya mwanadamu.
''Fanya kweli usibaki Nyuma'' ni Kauli mbiu ya Kampeni ya Mtu ni Afya hivyo kila Mwananchi anapaswa kufanya kweli ili kujilinda yeye na Familia Yake katika masuala ya Afya.
0 Comments