Aahidi kuisuka upya CUF, kupigania Katiba mpya
NA MWANDISHI WETU,
Chama Cha Wananchi (CUF) tayari kimepuliza kipyenga kuruhusu wanachama wake kujiandaa kwa ajili ya kutengeneza safu mpya ya uongozi.
Harakati mbalimbali zimeanza kwa wanachama wake kujipima ni nafasi zipi wanaweza kuzimudu katika kuendeleza mapambano ya kisiasa nchini.
Mmoja wa wanachama wake maarufu, Husna Mohamed ameitikia wito huo kwa kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Makamo Mwenyekiti wa chama hicho upande wa Zanzibar.
Husna amerejesha fomu ya kuomba ridhaa ya chama chake hicho leo Agosti 25, 2024 Mjini Unguja ambapo ameeleza sababu mahsusi za kuwania nafasi hiyo kuwa ni pamoja na kuhakikisha sauti za wanawake, vijana, na makundi yote yanapata fursa na utetezi stahiki ndani ya chama na Taifa kwa ujumla.
Husna ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF Taifa, amesema dhamira yake ya kugombea nafasi hiyo ni pamoja na kutanua wigo wa ushiriki wa wanawake na Vijana katika siasa za ndani ya chama na Taifa kwa ujumla.
"Kama tunavyojua, wanawake na Vijana tumekuwa chachu ya mabadiliko katika jamii, lakini bado nguvu na uwezo wetu haujatumika kikamilifu katika ulingo wa siasa. Nikiwa kama mama, dada, na mwana-harakati wa haki za wanawake, ninaamini kwa dhati kwamba, nafasi ya mwanamke siyo tu jikoni au nyumbani, bali ni pamoja na kwenye ngazi za maamuzi.
"Ni lazima tupewe nafasi sawa na za heshima katika vyombo vya uongozi na maamuzi ili tuweze kutoa mchango mkubwa katika kujenga chama chetu na Taifa lenye usawa, haki, na maendeleo.
"Ninaahidi kuendeleza jitihada za kuwawezesha wanawake wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kushiriki kikamilifu katika siasa na harakati za maendeleo." amesema Husna Mohamed
Katika hatua nyingine mgombea huyo wa moja ya nafasi za juu kabisa ndani ya chama cha CUF, ameahidi
kuhakikisha wanawake ndani na nje ya chama wanapatiwa elimu, mafunzo, na rasilimali zinazohitajika ili waweze kushindana kwa haki na wenzao wa kiume katika kugombea nafasi za uongozi.
Pia ameazimia kuhakikisha sauti za utetezi wa haki zinasikika kwa nguvu zaidi, hususan katika muktadha wa kutetea mageuzi na mabadiliko ya Katiba ya nchi ili iendane na mahitaji ya sasa na kuakisi matakwa ya wananchi, ikiwemo uwezo wa Zanzibar kudhibiti na kutawala mambo yake yenyewe zikiwamo raslimali zake.
"Nitapigania katiba inayozingatia usawa wa kijinsia, haki za binadamu, na demokrasia ya kweli.
"Ninaamini kwamba chama chetu cha CUF kinasimama kama chombo cha kuleta mabadiliko ya kweli, na ni jukumu letu kuhakikisha tunatoa msukumo wa kutosha ili kuhakikisha mchakato wa mabadiliko ya kikatiba unaendeshwa kwa uwazi, haki, na kwa kushirikisha wananchi wote."amesisitiza mgombea huyo.
Uchaguzi mkuu ndani ya CUF unatarajiwa kufanyika Septemba 25 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Mwisho
0 Comments