WATOTO waishio kwenye mazingira magumu kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha wamepatiwa misaada mbalimbali yenye thamani ya shilingi milioni 4.2
Misaada hiyo imetolewa leo na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha na wadau wa maendeleo ikiwemo benki ya CRDB.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa watoto hao kwenye sherehe ya makabidhiano iliyofanyika kwenye kituo cha Shallom kilichopo Kidenge Kata ya Mkuza Wilayani Kibaha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa alisema kuwa wako na watoto hao hivyo wasijione wapweke.
Shemwelekwa amesema kuwa wao na watoto hao ni familia moja hivyo wameamua kuwasaidia ili kuwapa faraja na amani hivyo wasijione wapweke na hakuna yatima na serikali inapenda watoto ndiyo sababu ikaweka elimu bure ili watoto wapate haki ya msingi ya kupata elimu.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mussa Ndomba amesema kuwa anapongeza wadau waliofanikisha kupatikana kwa misaada hiyo.
Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii Faustina Kayombo amesema kuwa Halmashauri ina makao tisa yenye watoto 601 na yote yamesajiliwa kisheria na kwa upande wa mafanikio ni makao kuwa na majengo bora.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mahitaji ya shule, magodoro, madaftari, kalamu, penseli, vichongeo, rula, mafuta ya kujipaka, mafuta ya watu wenye ualbino.
mwisho
0 Comments