Ubalozi wa Uingereza Nchini Tanzania umeahidi kufanya kazi kwa karibu na waandish wa Habari wote Nchini wakiwemo wa wale wa Mkoa wa Mwanza.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Idara ya Siasa na Utawala Bwana Samuel Raff toka ubalozi wa Uingereza alipoitembelea klabu ya waandishi wa habari ya Mkoa wa Mwanza (MPC) na kuongea na viongozi na baadhi ya wanachama wa MPC.
Bwana Raff amesema kuwa, Uingereza inatambua kazi kubwa inayofanywa na MPC kupitia wanachama wake kwenye kutafuta, kuchakata na kutoa taarifa kwa jamii.
" Tunaona kazi zenu mnazofanya hasa kwenye kuandika habari za uwajibikaji na kuijenga jamii iliyo bora, kwa kweli tunawapongeza sana" Alisema Raff.
Raff pia alieleza mipango ya Serikali ya Uingereza kwenye kuanzisha program ya Asasi za Kiraia na vyombo vya habari ijulikanayo kwa jina la wajibika itakayozinduliwa mwakani 2025.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi Sylivester Ernest toka Idara ya Siasa na Utawala aliwataka waandishi wa habari wa Tanzania kuchangamkia fursa ya kimasomo zinazotolewa na ubalozi wa Uingereza Nchini.
" Miimi pia ni Mwandishi wa Habari mwenzenu na nilinufaika na fursa hizo, hivyo naomba mchangamkie fursa hizo" Alisema Ernest.
Naye Mwenyekiti wa MPC Bwana Edwin Soko aliiomba Uingereza kuongeza fursa za waandishi wa habari kujengewa uwezo ili waweze kufanya kazi zao kwa weledi.
Ziara hiyo ya maafisa wa Uingereza imefanyika leo kwenye ofisi za MPC jijini Mwanza.
0 Comments