Na Matuko Daima Media, Dar es Salaam
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Educate! leo Julai 8, 2024 wameingia makubaliano ya kushirikiana kwa miaka sita katika utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa ikiwamo katika somo jipya la Elimu ya Biashara ambalo ni la lazima kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
Katika hafla ya makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk. Aneth Komba amesema kuwa , makubalino hayo yamekuja wakati muafaka na kwamba somo la Elimu ya Biashara litawasaidia wanafunzi nchini kujiajiri mara baada ya kuhitimu masomo yao.
“Tunashukuru wenzetu wa Educate! kwa kuendelea kushirikiana nasi katika kuhakikisha somo la Elimu ya Biashara linafundishwa katika viwango vya juu wakati huu wa kutekeleza Mtaala ulioboreshwa”amesema.
Dk. Komba ametaja maeneo kadhaa waliyokubaliana kushirikiana na Educate! ni kutoa mafunzo kwa walimu kazini wa somo la Elimu ya Biashara katika kutekeleza mtaala ulioboreshwa, kuajiri walimu wa Elimu ya Biashara kwa mkataba katika shule za sekondari ambazo zitakuwa na uhaba wa walimu wa masomo hayo, na maeneo mengine.
Kwa upande wake ,Mkurugenzi Mkaazi wa Mahusiano wa Educate!, Kamanda Kamiri amesema kuwa wao wataendelea kushirikiana na TET katika kuhakikisha somo la Elimu ya Biashara nchini linafundishwa na kueleweka kwa wanafunzi ambao wanatarajiwa kufanya vyema katika eneo la ujasiriamali.
“Ni jambo jema kwetu kuendelea kushirikiana na TET katika eneo la ufundishaji na ujifunzaji wa somo la Elimu ya Biashara kwa wanafunzi wa Tanzania" amesema Kamiri.
0 Comments