NA JOSEA SINKALA, SONGWE.
Katibu tawala wa mkoa wa Songwe Happiness Seneda, amewataka wananchi kuchukia vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo kwa watoto.
Seneda ametoa rai hiyo wakati akifunga kongamano la uwezeshaji wanawake kiuchumi katika mkoa wa Songwe kufuatia taarifa ya dawati la jinsia mkoa wa Songwe kuonyesha kuwa bado mkoa huo bado unaghubikwa na vitendo mbalimbali vya ukatili, unyanyasaji na ulawiti.
Kiongozi huyo mtendaji wa mkoa, amewataka wanaume kuacha kuwafanyia vitendo vya ukatili wanawake na watoto wa kike na kuwasababishia ujauzito akisema wanawake wapo wa kutosha.
"Jamani wanawake wa Songwe wakubwawakunwa si wapo wengi! Tena hata hapa nawaona wengine hawana hata pete tena wazuri kabisa sasa kwanini wanaume wanaenda kwa watoto, sasa kupitia jukwaa hili tutume ujumbe wanaume tuachieni watoto watu wazima wapo acheni watoto wasome", amesema RAS wa Songwe Happiness Seneda.
Katibu tawala huyo amewataka wanawake (wazazi na walezi) pamoja na kujikita kwenye utafutaji wahakikishe wanakuwa makini na watoto wao ili kuwalinda na vitendo mbalimbali vya ukatili.
Kwa upande wake mkaguzi wa Polisi Debora Mhekwa kutoka dawati la jinsia mkoa wa Songwe, amesema mkoa wa Songwe inakabiliwa na matukio mbalimbali ya ukatili ikiwemo wa kiuchumi, kihisia na kimwili.
Mkaguzi huyo wa Polisi amewataka wanawake na wanaume kwa ujumla kuachana na matendo ya ukatili, unyanyasaji na ulawiti ikiwemo kwa watoto badala yake kuwalinda watoto ili watimize ndoto zao na kuwa na kizazi imara sasa na baadaye.
0 Comments