Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amewataka wananchi wa Zanzibar kujiandaa na mabadiliko ya Serikali mwaka 2025, huku akiwaahidi kwamba yeye atausimamia ushindi wao katika Uchaguzi Mkuu ujao na kuiongoza Zanzibar Mpya.
Akifafanua kauli yake hiyo, Mheshimiwa Othman amewahakikishia wananchi kwamba suala la kura ya siku mbili halitokuwepo na badala yake kura zitapigwa siku moja na maamuzi yao kuheshimiwa.
Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameyasema hayo leo Jumapili, Julai 21, 2024 wakati alipokuwa akiwahutubia viongozi, wanachama, wapenzi na wafuasi wa Chama chake, akiwa Mgeni Rasmi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika Uwanja wa Mpira wa Mwenge Sports Club, huko Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja.
Akizungumzia hali ngumu za maisha zinazowakabili Wazanzibari, amesema hujuma zinazofanywa na watawala zinaendelea kuleta umasikini na kuifanya nchi kukosa mwelekeo kwa kuwepo viongozi wasiokuwa na uzalendo na wasiowajali wananchi.
Amesema kumkosesha mwananchi kitambulisho cha ukaazi na kile cha kupigia kura ambacho ni haki yake kikatiba na kisheria ni uadui kwa wananchi na ni usaliti mkubwa.
"Viongozi wa namna hii ambao wanathamini matumbo yao badala ya maslahi ya wananchi ni 'wahaini', na ni wazi tunatakiwa tushikamane tuwaweke pembeni ili tupate fursa ya kurudisha hadhi na thamani ya watu wetu na nchi yetu," alisisitiza Mheshimiwa Othman.
Naye Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Zanzibar), Ndugu Ismail Jussa, akitoa salamu zake kwenye Mkutano huo
amesema umasikini unaowakabili wananchi wa Zanzibar unatokana na ufisadi wa baadhi ya viongozi wanaotawala sasa ambao hutumia pesa za Wazanzibari katika miradi isiyotekelezeka huku wakiwaacha wananchi katika ugumu wa maisha.
Pia alisisitiza kwamba mamlaka kamili ya Zanzibar hayaepukiki kwa maslahi mapana ya Zanzibar na Wazanzibari.
"Si haramu kwetu kuisemea na kuitetea Zanzibar, kwani hii ni nchi yetu na huu ni wajibu wetu mpaka turejeshe mamlaka kamili ya nchi hii", alisema.
Awali, wakitoa salamu za wananchi wa Kusini Unguja, Ndugu Khatib Juma (Chaki), Ndugu Shaaban Khamis Abdalla na Bi Ziada Mwadini Mussa, wamesema Mkoa huo ulikuwa unajiweza kiuchumi ila maendeleo na utajiri uliokuwepo katika Mkoa wa Kusini Unguja wote umepotea kutokana na kutokuwepo usimamizi bora wa viongozi wanaotawala, huku wakieleza changamoto ya miundombinu, hali duni za maisha, ukosefu wa ajira, usumbufu wa kupata vyeti vya kuzaliwa na changamoto za ardhi kukabidhiwa wawekezaji, pamoja na kuwataka wananchi kuungana pamoja kwa dhamira ya kuikomboa Zanzibar na kuirudisha katika hadhi yake.
Katika Mkutano huo, Mheshimiwa Othman aliwapokea wanachama wanane (8) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliokihama chama hicho na kujiunga na ACT Wazalendo.
Viongozi wa ngazi mbali mbali wa Chama hicho wakiwemo Wajumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu, Wabunge na Wawakikishi wamehudhuria Mkutano huo.
Mkutano huo ulitanguliwa na burudani mbali mbali zikiwemo sarakasi, utenzi na nyimbo za wasanii wa kizazi kipya (mguu mbele mguu nyuma).
Mapema asubuhi kabla ya mkutano huo, Mheahimiwa Othman alipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na wazee wa Kusini Unguja ikiwa ni sehemu ya kusikiliza changamoto zao. Kikao hicho kilifanyika katika Ukumbi wa Mitihani wa Skuli ya Kizimkazi Dimbani, pamoja na kutoa mkono wa pole kwa Sheikh Abdulkadir Mohamed (Kitisho) wa Kumbini, Makunduchi.
0 Comments