Na Fadhili Abdallah,Kigoma
HALI ya sintofahamu imewakumba wananchi wanaoishi kuzunguka bonde la Nyankara kitongoji cha Pamila Kijiji cha Pamila kata ya matendo halmashauri ya wilaya ya Kigoma kufuatia kuibua ujiji tope zito linalodhaniwa kuwa ni volcano.
Wananchi na viongozi wa kijiji hicho wakizungumza mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya Kigoma ikiongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo,Salum Kali walisema kuwa hali hiyo ilianza pole pole lakini mwishoni mwa wiki iliyopita tope hilo liliongezeka na kufunika eneo kubwa la bonde hilo.
Obedi Tuwazaniwe mwenyekiti wa kijiji cha Pamila halmashauri ya wilaya Kigoma alisema kuwa alipata taarifa ya hali hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita kutoka kwa wananchi wakieleza kuwepo kwa ongezeko kubwa la tope linalodhaniwa kuwa ni volcano na hivyo kuanza kutoa taarifa kwa mamlaka za serikali.
Kwa upande Kaimu Afisa Mtendaji wa kijiji cha Pamila Peter Edward alisema kuwa taarifa zinazonyesha kuwa hali hiyo ilianza baada ya mtu mmoja aliyeanzisha bwawa la kufuga Samaki katika eneo hilo lakini Samaki wote walikufa na kati kati ya bwawa alilokuwa akitumia kufugia samaki kuibuka kichuguu kikubwa.
Alisema kuwa baada ya muda kichuguu hicho kiliongezeka lakini pia kukiwepo na mchanga wenye maji maji sawa na tope zito hivyo watu wengi kuanza kupata hofu kwamba huenda eneo hilo kukalipuka volcano kama inavyotokea maeneo mengine hivyo kulazimika kutoa taarifa kwa mamlaka za serikali.
Akizungumza hali hiyo Mtaalam wa Miamba na jiolojia kutoka ofisi ya madini mkoa Kigoma, David William Ndosi alikiri kuwa hiyo ni volcano ya mchanga na maji ambayo kitaalam inajulikana kama Sand Eruption Volcano ambayo tope na maji hayo hayana moto kama ilivyo volcano nyingine zinazojulikana sana na watu.
Ndosi alisema kuwa kwa sehemu kubwa volcano kama hiyo inatokea kwenye maeneo yenye bonde la ufa na matetemeko kutokana na miamba kutikiswa hivyo mchanga na chembe chembe za maji zinazotengeneza tope kupanda juu kama ilivyotokea eneo hilo.
Hata hivyo alisema kuwa tope hilo halina madhara lakini wananchi wanapaswa kukaa mbali kwani wanaweza kuzama na kupoteza Maisha huku akieleza kuwa uchunguzi Zaidi wa kimaabara utafanywa kujua sababu hasa ya kilichotokea.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi wa Baraza la Taifa la utunzaji mazingira (NEMC),Edith Makungu alisema kuwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa Mkuu wa wilaya Kigoma wamefika eneo la tukio na wameshachukulia sampuli za maji na udongo kwa ajili ya uchunguzi ili kujua kama yana madhara au vipi.
Akizungumza katika eneo hilo Mkuu wa wilaya Kigoma,Salum Kali alisema kuwa alipata taarifa hiyo juzi kutoka uongozi wa serikali ya Kijiji cha Pamila hivyo kuongozana na kamati ya ulinzi na usalama kutembelea eneo hilo akiwa na wataalam wa ofisi ya madini na NEMC.
Sambamba na hilo Mkuu huyo wa wilaya amewaonya watu wote kukaa mbali nae neo hilo ili kuzuia madhara yeyote yanayoweza kujitokeza ambapo wataalam wameanza kazi ya kufanya uchunguzi wa kile kilichosababisha hali hiyo.
Mwisho.
0 Comments