Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Waandishi wa habari mkoani Njombe wametakiwa kutumia ripoti ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali katika utekelezaji wa majukumu yao,ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo na kwa ubora unaotakiwa kulingana na thamani ya fedha inayotolewa na serikali.
Ofisa Mahusiano Serikalini Ofisi ya Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG), Focus Mauki Anatoa kauli hiyo wakati akitoa mafunzo kwa wanahabari wa mkoa wa Njombe namna ofisi ya taifa ya ukaguzi inavyotekeleza majukumu yake, ambapo amewataka kutumia ripoti hiyo kuanzia kwenye ngazi ya mitaa na vijiji ili miradi hiyo itekelezwe kwa wakati na ianze kutoa huduma kwa wananchi.
Mauki amesema ikiwa waandishi wa habari watafanya hivyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uwajibikaji kwa watendaji wa serikali na kuondoa vitendo vya ubadhirifu wa fedha za umma.
Aidha mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Njombe, Damian Kunambi amesema kupitia mafunzo hayo yatawasaidia wanahabari kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao huku akizitaka halmashauri kutoa ushirikiano pindi zinapohotajika.
Nao baadhi ya wanahabari mkoani Njombe akiwemo Gabriel Kilamlya na Linah Sanga ambaye ni Ofisa habari wa halmashauri ya mji wa Makambako wamesema watayatumia mafunzo hayo kuandaa na kuripoti habari zenye tija kwa jamii.
Hatua ya kuwajengea uwezo wanahabari katika kufanya uchambuzi wa kina na kuripoti habari zinazotokana na ripoti ya CAG Kutasaidia pia kuzikumbusha mamlaka zenye wajibu wa kutekeleza miradi ya serikali ambayo imekwama ili hali serikali imepeleka fedha.
Damian Kunambi Mwenyekiti wa Njombe Press Club
0 Comments