Katika kuhitimisha ziara yake ya siku tano Mkoani Mara, leo tarehe 29 Julai, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Ado Shaibu amekutana na Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi na kuwasilisha kwake changamoto za wananchi zilizoibuliwa kwenye ziara yake.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, hoja zilizowasilishwa zinahusu; changamoto kwenye malipo ya TASAF; migogoro ya ardhi baina ya wananchi na hifadhi (Serengeti) na migodi (Nyamongo); ubadhirifu kwenye miradi mbalimbali ya huduma za kijamii kama vile ujenzi chini ya kiwango wa Kituo cha afya Kyang'ombe (Rorya) na ubadhirifu katika mradi wa shule ya Sekondari katika Kata ya Mugango (Musoma Vijijini); fidia kwa wananchi wa Utegi Farm (Rorya), Uwanja wa ndege (Musoma Mjini) na Mradi wa EPZ (Bunda).
Pia, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo ametoa rai kwa Mkuu wa Mkoa kuwa na mkakati wa kufufua viwanda vya kuchambua pamba, nyama, samaki na maziwa ambavyo miaka ya nyuma vilisaidia sana kutoa ajira na kukuza uchumi wa Mara.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Ado Shaibu, Mkuu wa Mkoa Mara amezipokea changamoto zilizowasilishwa na kuahidi kuzifuatilia ili kubaini ukweli wake na kuzifanyia kazi.
0 Comments