Header Ads Widget

DC KASILDA AKERWA NA RUWASA KUTOSHIRIKIA NA JAMII.

 


NA WILLIUM PAUL, SAME. 


MKUU wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni ameeleza kusikitishwa na kitendo cha Wakala wa maji safi na usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) wilayani humo kushindwa kushirikisha jamii husika kwenye maeneo mbalimbali ambako kunatekelezwa miradi ya maji hali inayopelekea kutokea malalamiko kutokana na kutoelewa nini kinaendelea.


Kasilda ameeleza hayo baada ya malalamiko ya wakazi wa Kijiji cha Bangalala kwenye mkutano wa hadhara wakidai kusitishiwa huduma ya maji kwenye jumuiya ya watumia maji Mhetute takribani miezi mitatu pasipo kupatiwa taarifa yeyote kutoka kwa mamlaka husika.



"Waziri wa Maji Jumaa Aweso yupo vizuri sana lakini tukija huku chini mnamuangusha sana, yani lazima mbadilike RUWASA haiwezekani ulete mradi kwenye Kijiji halafu wananchi wa eneo husika hawajui chochote kuhusu huo mradi". Alisema Kasilda. 


Aidha amemuagiza Afisa Tarafa ya Mwembe Mbaga, kuitisha mkutano wa hadhara ndani ya wiki moja kutekeleza takwa la kisheria kuchagua viongozi watakao simamia mradi huo kuwa na matumizi endelevu, ambapo pia husaidia kudhibiti kuhujumiwa kwa miradi inayotekelezwa kwani wananchi watakuwa na ufahamu juu ya utekelezaji wake.



Kwenye mkutano huo baadhi ya wananchi wamesema kuwa..."Sisi hatuelewi chochote kuhusina na maendeleo ya huu mradi wa Mhetute, tunaona wataalam kutoka RUWASA wanakuja saiti wanang'oa gati maji hayatoki kabisa lakini baadae wanakuja kudai hela za maji wakati tumesitishiwa huduma na wananchi tunatumia maji kutoka mtoni huko"....


"Hii ukiangalia ni kero kubwa sana kwa wananchi wa Bangalala, ukiangalia pale kwenye mradi wa Mhetute ni uzembe wa mtu mmoja kushindwa kulipia maji wao wanakuja hawatoi taarifa wala kuuliza chochote wanang'oa gati wanaondoka, hatukatai kulipia maji lakini tunachoomba kama kunamabadiliko tupewe taarifa kwasababu ni haki sisi kulipia maji endapo tukiwa tumetumia"....


Kwaupande wake Meneja wa Jumuiya hiyo Octavian Ulomi amesema kituo hicho kimefungwa kutokana na kukosa mtu wa kusimamia ambaye atakuwa anakusanya fedha za watumiaji maji hayo.


"Nilimuachia jukumu fundi msaidizi kwamba akitokea mtu ambaye anataka kusimamia kile kituo aje Ofisini tuongee vizuri tukikubaliana basi tutakifungua kwa sababu sasa hivi maji ni ya kulipia na tunalipia kwa asilimia chache ambapo kati ya ndoo tano tunalipia shilingi mia". Alisema Ulomi. 


Mwisho.. 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI