Header Ads Widget

WAKILI MWABUKUSI AIANGUKIA SERIKALI KUTOWAPATIA VIWANJA WAATHIRIKA WA MAPOROMOKO YA TOPE MLIMA KAWETELE MBEYA.

 


NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Wakili wa kujitegemea Boniface Anyisile Mwabukusi ameitaka Serikali kuingilia kati na kudhamiria kuwahamisha wananchi waliothirika na maporomoko ya tope katika eneo la mlima Kawetele Kata ya Itezi Uyole jijini Mbeya kwa kuhakikisha wananchi hao wanapewa maeneo mengine rafiki kwa ajili ya kuendesha maisha yao.


Wakili Boniface Anyisile Kajunjumele Mwabukusi, amesema hayo baada ya kuwatembelea waathirika hao katika kambi ya Shule ya msingi Tambukareli Kata ya Itezi jijini Mbeya ambapo Serikali imetenga ili watu hao kuishi kwa muda wakati taratibu nyingine zikiendelea.


Pamoja na hayo amekabidhi sehemu ya mchango wake ambao ni mchele na mafuta ya kupitikia ili kuwatia moyo wananchi hao kwenye kipindi kigumu wanachopitia.


Amesema ni wajibu wa wadau na mtu mmoja mmoja katika jamii kwenda kuwatembelea waathirika wa maporomoko hayo na kuwafariji kwa vitu walivyo navyo huku wajibu mkubwa wa Serikali ukiwa ni kuhakikisha inatafuta eneo lingine rafiki ili wananchi hao wakaanzishe makazi ikiwa ni pamoja na kuwajengea makazi ya muda kama walivyofanya kwa wakazi wa Ngorongoro waliohamishwa kwenda Msomera Mkoani Tanga.


Naye Mwenyekiti wa Baraza la wazee wa CHADEMA (BAZECHA) Mkoa wa Mbeya David John Mwambigija ameeleza masikitiko yake kwa Serikali ambayo walipima viwanja hivyo ambavyo vipo bondeni na milimani hivyo wananchi wake wanapokumbwa na maafa ni wajibu wa Serikali kuwahamisha ili kuendelea kulitumikia Taifa lao.


Kwa upande wake aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Jimbo la Mbeya mjini Judith Mwampiki, pamoja na mchango wake kwa wananchi hao, ameitaka Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kutupia jicho waathirika hao ili kwenda kuanzisha makazi yao ya kudumu mahali salama.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS