NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Baraza la vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA (BAVICHA) Wilaya ya Mbeya, limemchukulia fomu ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa aliyekuwa Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi (Sugu).
Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu hiyo na katibu wa Kanda ya Nyasa Gwamaka Mbughi kwa niaba ya Katibu mkuu wa CHADEMA Taifa John Mnyika, Mwenyekiti wa vijana wa CHADEMA Wilayani Mbeya Richard Sosten, amesema Kanda ya Nyasa inahitaji mabadiliko na vijana wa Wilaya yake na majimbo jirani wanaamini Joseph Mbilinyi atawavusha katika Kanda hiyo.
Mwenyekiti huyo amesema Nyasa inahitaji mabadiliko kutoka alipoishia mtangulizi wake (Simon Msigwa) hivyo amesema Mbunge huyo wa zamani atakifaa Chama hicho cha upinzani katika kukisimamia ili kutimiza malengo yake ya kushika dola.
Naye Mwenyekiti wa BAVICHA Jimbo la Mbeya mjini Hassan Mwamwembe, amewashukuru viongozi na vijana mbalimbali vijana wa CHADEMA walioungana nao ili kwa pamoja kumchukulia fomu mtia nia huyo wa nafasi ya uenyekiti wa CHADEMA ngazi ya Kanda yenye mikoa mitano ya Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa na Songwe.
Joseph Osmund Mbilinyi (Mr. II Sugu) ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati kuu ya CHADEMA Taifa na aliyewahi kuwa Mbunge wa Mbeya mjini ana kibarua cha kupambana na Mchungaji Peter Simon Msigwa ambaye alikuwa Mbunge wa Iringa mjini anayetetea nafasi hiyo ya uenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa ambapo CHADEMA kinaendelea kusuka timu yake ya viongozi na sasa ni katika ngazi ya Kanda nne za awali na baadaye katika Kanda nyingine sita ili kuhakikisha kinapata viongozi wengine watakaoongoza Chama hicho na mabaraza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo (2024 - 2029).
0 Comments