Header Ads Widget

TARI YAENDELEA KUTOA ELIMU KWA WAKULIMA NCHINI KUHUSU KANUNI BORA ZA UZALISHAJI ZAO LA ALIZETI





Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA 

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kituo cha  Ilonga kilichopo Kilosa mkoani Morogoro imeendelea kutoa elimu kwa wakulima nchini kuhusu kanuni bora za uzalishaji wa zao hilo ikiwemo matumizi ya mbegu bora ya Record kwa lengo la kuongeza tija ya uzalishaji na kipato. 

Mtafiti na Mhaulishaji wa Teknolojia za Kilimo kutoka TARI ILONGA, Baraka Daniel, akizungumza na wakulima na viongozi wa kijiji cha Mdilu kata ya Mwasauya Halmashauri ya Singida,katika siku ya mkulima wa alizeti alisema mbali na mbegu ya Record mbegu nyingine mpya zilizofanyiwa utafiti ambazo zimetambulishwa kwa wakulima waanze kuzitumia ni TARI ILO-19  na TARI NAL-19.

Daniel alisema wanahamasisha matumizi ya mbegu hizo kwasababu zinastahimili mabadiliko ya tabia-nchi, bei ya wastani ambayo wakulima wengi wanamudu kununua pia zina tija katika uzalishaji.


Alisema Mkoa wa Singida ni kati ya mikoa nchini inayolima zao la alizeti lakini tija ni ndogo kutokana na wakulima wengi kutumia mbegu za kienyeji ambazo hazijafanyiwa utafiti hivyo wakulima wahamasike kutumia mbegu bora.

Naye Mratibu wa Upimaji wa Afya ya Udongo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya  Singida, Benny Joel, alisema katika kuadhimisha siku ya mkulima wa alizeti wanatoa elimu kwa wakulima ili kutambua umuhimu wa upimaji afya ya udongo kwa lengo la kuongeza uzalishaji.


"Upimaji wa afya ya udongo ndio nguzo ya kuongeza uzalishaji katika kilimo cha alizeti na utamsaidia mkulima kufahamu upungufu uliopo katika shamba lake na virutubisho vilivyopo na namna gani ya kuboresha udongo wake na kumshauri mkulima  namna kutumia mbolea kuongeza rutuba," alisema.


Joel alisema wakulima wanapaswa kuzingatia upimaji wa afya ya udongo kwani serikali kupitia Wizara ya Kilimo imetoa vifaa kwa ajili ya kupima afya ya udongo ambao utawezesha kuongeza uzalishaji kutoka tani 0.7 hadi kufikia tani 1.4 kwa shamba lenye ukubwa wa hekari moja.

Alisema awali wakulima walikuwa wanapata kati ya gunia 5 hadi 7 za kilo kwa ekari moja kwasababu zoezi la upimaji wa udongo lilikuwa halijafanyika na pia mbegu walizokuwa wanatumia wakulima ni za kienyeji na pia matumizi ya mbolea hayakuwepo.



Kwa upande wao wakulima wa alizeti walisema tangu waanze kutumia mbegu ya alizeti aina ya Record kwa hivi sasa wanapata gunia 12 hadi 14 za kilo 60 kwa ekari moja wakati awali walipokuwa wanatumia mbegu za kienyeji walikuwa wanapata gunia 4 hadi 5.

"Mbegu hii ya Record ambayo tunaipata kutoka TARI na Wakala wa Mbegu za Serikali (ASA) imetusaidia sana kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti na tunaiomba serikali iwe inatuletea mbegu hii kila msimu wa kilimo," walisema Maria Mandi na Rashid Idd ambao ni wakulima wa alizeti wa kijiji cha Mdilu.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Mdilu,Samson Samweli, alisema mbegu ya Record imekuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima wa kijiji chake kutokana na kuongeza uzalishaji ambao kupitia zao hilo wameinua hali zao za maisha.
MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS