Header Ads Widget

MRADI WA AFYA YANGU WATAJWA KUIBUA WATU 700 WENYE VVU KILA BAADA MIEZI MITATU

Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA 

 

MRATIBU WA MRADI WA USAID AFYA YANGU,SAID MGELEKA

 


MRADI wa USAID Afya Yangu ambao unatekelezwa mkoani Singida, umefanikiwa kuibua  watu wapya zaidi ya 700 wenye maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na 600 wa kifua kikuu ambao wanaibuliwa kila baada ya miezi mitatu.

Meneja wa mradi huo Mkoa wa Singida, Said Mgeleka, alisema hayo jana wakati wa kikao cha kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi ambao umeanza kutekelezwa tangu Novemba 2021 katika mikoa ya Dodoma, Manyara, Arusha,Tabora, Kilimanjaro na Singida.

Alisema wateja walioibuliwa kwa kugundulika kuwa na VVU wamesaidiwa kuanzishiwa Dawa za Kufubaza Virusi (ARVs) ili wasiweze kupata madhara zaidi na hivyo kuilinda jamii ambapo kama wasingeanza kutumia dawa hizo wanaweza kuwaambukiza watu wengine zaidi.

Mgeleka alisema kwa upande wa watu wanaoibuliwa wakiwa na ugonjwa wa kifua kikuu wanasaidiwa matibabu na vipimo ambapo baadhi yao wamepata ahuweni na wengine kupona kabisa.

Alisema kwa upande wa uzazi wa mpango kila baada ya miezi mitatu mradi huo umekuwa ukiwaibua zaidi ya wateja 1200 ambao hupatiwa njia za uzazi wa mpango za kisasa na pia katika kipindi hicho wanawake 1200 hufanyiwa uchunguzi kubaini kama wana viashiria vya ugonjwa wa saratani ya mlango wa uzazi 

         KATIBU TAWALA MKOA WA SINGIDA, DK.FATUMA MGANGA


Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk Fatuma Mganga, akifungua kikao hicho aliwaagiza Waganga Wakuu wa Wilaya na wadau wengine wa afya kuwatafuta na kuwarejesha katika matumizi ya dawa za kufubaza makali ya virusi vya ukimwi waathirika 857 ambao wameacha kutumia dawa hizo.

Waathirika hao walioacha kutumia dawa za ARV  wanatoka katika Halmashauri za Wilaya ya Ikungi,Singida na Itigi.

Dk.Mganga alionesha kutoridhishwa na idadi hiyo kubwa ya watu wanaotuma dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kuacha kutumia dawa hizo na amesisitiza kuwekwa mikakati na mipango madhubuti itakayosaidia kurejesha kundi hilo katika matumizi ya ARV dawa haraka iwezekanavyo.

Alisema kuna umuhimu wa kutengeneza mahusiano mazuri kati na watoa huduma na wateja wao ikiwemo kuwapigia simu pindi wanapoona mteja wao hafiki kuchukua dawa ili kujua sababu ambazo zinamfanya asiende kuchukua dawa hizo ili kuona namna bora ya kumsaidia.

     MGANGA MKUU WA MKOA WA SINGIDA, DK.VICTORINA LUDOVICK


Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Victorina Ludovick, ametaja sababu zinazopelekea idadi kubwa ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI mkoani hapa kuacha kutumia dawa za kufubaza virusi kuwa ni waathirika hao kuhama na kwenda maeneo mengine na umbali kutoka kwenye makazi yao hadi kwenye vituo vya kutolea huduma hizo.

Ludovick alisema mpango uliopo kwa sasa ni kuhakikisha watumiaji hao wa dawa hizo wanatafutwa popote walipo na kuwapa ushauri nasaha kuhusu umuhimu wa matumizi ya dawa hizo kwa ajili ya afya zao


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS