NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Vunjo, Dkt Charles Stephen Kimei ameendelea na ziara yake katika jimbo hilo ambapo amekagua ujenzi wa mradi mkubwa maji katika kata ya Marangu Mashariki (Vijiji 02) na Mwika Kaskazini (vijiji 06) utakaohudumia vijiji nane vya kata hizo na ambao unagharimu Bilioni 1.8
Akizungumza na viongozi pamoja na wananchi wa kijiji cha Msae Kinyamvuo mara baada ya kukagua ujenzi huo, Kimei amesema mradi huo ni kielelezo cha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwatua ndoo kichwani wakina mama wa Jimbo la Vunjo.
"Huu ni kati ya miradi mikubwa katika jimbo letu ni mradi ambao unakwenda kumaliza changamoto ya maji katika kata zetu mbili za Mwika Kaskazini, Mwika Kusini tuna kila sababu ya kumshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake kwetu wananchi wa Mlimba" Alisema Dkt Kimei.
Na kuongeza "Napenda kutumia fursa hii pia kuwapongeza sana Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA kwa juhudi na kazi nzuri wanayoifanya ya kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi na nitoe rai kwa MUWSA wanaotekeleza ujenzi wa mradi huu kutambua kwamba ni kiu yetu wananchi wa kata hizi za Marangu Mashariki (Vijiji vya Rauya na Samanga) na Mwika Kaskazini (vijiji vyote 6 - Mrimbo Uuo, Marera, Nganyeni, Lole, Msae Kinyamvuo na Maring'a) kuona tunapata maji hivyo wakamilishe mradi huu kwa haraka ili wananchi sasa waepukane na changamoto za gharama za ziada kununua maji na kutembea umbali mrefu kufuata maji".
Aidha Mhandisi Deo kutoka MUWSA anayesimamia miradi hii ya maji ameeleza ya kwamba MUWSA imejipanga kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kupata huduma.
Pia ameeleza wakati wowote mwezi Aprili, 2024 MUWSA wataanza uchimbaji wa kisima katika kijiji cha Kirueni kata ya Mwika Kusini pamoja na ujenzi wa tenki kubwa hali itakayoimaliza kabisa kero ya maji katika kata hiyo.
Naye Diwani wa kata ya Mwika Kaskazini Samwel Shao amemueleza kama lipo jambo la kukumbukwa na wananchi wa kata hiyo kwake pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan ni kumalizwa kwa kero ya maji pale mradi huu mkubwa utakapokamilika.
Dkt Kimei amekuwepo Jimboni kwa siku tatu sasa akikagua miradi pamoja na vikao na wadau wa maendeleo.
Mwisho...
0 Comments