Waislamu wanasherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr ambayo inaadhimisha mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Lakini mwaka huu vita huko Gaza vimeleta huzuni kwenye sherehe hizo, haswa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.
Wito wa adhana unasikika katika mitaa ya mji mkongwe wa Jerusalem Mashariki unaokaliwa kwa mabavu – wakati ukipita katika kituo cha ukaguzi cha Israel kabla ya kufika kwenye mlango wa nyumba ya Ilham mwenye umri wa miaka 35.
"Unasikia hiyo adhana?" anauliza kwa furaha. "Inatoka al-Aqsa."
Msikiti wa Al-Aqsa - mojawapo ya maeneo matakatifu zaidi katika Uislamu – upo karibu na nyumba yake.
Msikiti upo katika eneo linaloshindaniwa - likijuulikana kama Temple Mount, ambalo ni takatifu zaidi katika Uyahudi.
Ni fakhari kubwa kwake kuishi hapa.
"Ni zawadi ya kiroho," anasema. "Kila mtu ananionea wivu kwa hilo. Wananiambia, 'Una bahati sana!'
Mfanyakazi huyo wa kijamii ni mmoja wa Wapalestina wenye asili ya Afrika (Afro-Palestinians) wapatao 450, kutoka kizazi cha mahujaji kutoka Chad, Nigeria, Senegal na Sudan, wanaoishi katika eneo hili la Waislamu ndani ya mji mkongwe
Nyumba zao ziliwahi kuwa magereza yaliyotumiwa na Dola la Otman kabla ya Uingereza kuchukua udhibiti wa Jerusalem mwaka 1917.
Miaka kadhaa baadaye, baada ya Uingereza kufanya jaribio lililoshindwa la kumuua Mufti Mkuu wa Jerusalem, Sheikh Haj Amin al-Husseini, alitoa ardhi hiyo kwa jumuiya ya Wapalestina wenye asili ya Afrika kama ishara ya nia njema.
Mlinzi kutoka jamii hiyo ndiye aliyeokoa maisha ya Mufti, na akapoteza maisha yake katika tukio hilo.
Jumuiya hiyo, ambayo imeishi katika eneo hilo kwa vizazi vitatu hadi vinne, sasa inajulikana kuwa walinzi wa al-Aqsa.
Mwaka huu, Ilham anasema, hakuna furaha yoyote inayoweza kuchukua nafasi ya unyonge wa Waislamu wa Palestina wanaoishi Jerusalem Mashariki.
"Unaweza kusema, 'Eid Njema,' na kukusanyika na kuketi na familia, lakini Eid gani?" Anauliza. "Hakuna Ramadhani, hakuna Eid. Kila kitu hakiko kama ilivyokuwa, katika maisha yetu ya kila siku. Tunakaa tu na kufikiria Gaza."
0 Comments