Header Ads Widget

WATUMISHI SINGIDA WAASWA KUTUMIA MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI KUTOA HUDUMA KWA WANANCHI

  




Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA


SERIKALI Mkoa wa Singida imewataka watumishi wa umma na watu binafsi kutumia Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) katika kutoa huduma kwa wananchi kwa kuwa unarahisisha utoaji na ufikishaji wa huduma kwa urahisi na kuondoa usumbufu wa kutumia gharama kufika katika ofisi za Serikali.


Mkuu wa Wilaya ya Singida,Godwin Gondwe, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amesema hayo leo (Machi 22,2024) wakati akifunga mafunzo kuhusu anwani za makazi kwa watumishi wa serikali,taasisi binafsi na viongozi wa dini yaliyofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.


"Kila mfanyakazi wa serikali ambaye unajua kwamba unatoa huduma kwa wananchi ni muhimu sana na ni wajibu kupakua app ya NaPA ili kuweza kurahisisha katika ufuatilia na ulipaji wa kodi na kupata mapato yetu na hivyo kufikisha huduma kwa wananchi," amesema


Gondwe amesema suala la  Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) linatakiwa kuchukuliwa kwa umuhimu wa kipekee sana kwani itafika wakati mtu anaweza kupata huduma  serikalini au sehemu yeyote akiwa nyumbani kwake kwa kuingia kwenye mtandao wa NapA.


"Sisi kama viongozi wa serikali tunatakiwa kutoa huduma kwa wananchi kwa kutumia mfumo wa NaPA na mtakumbuka Rais Samia Suluhu Hassan amezengumzia sana kutatua kero na changamoto za wananchi na ametoa minara ili tuweze kuwahudumia wananchi kwa haraka kwani hivi sasa dunia inakwenda kwa kasi sana," amesema Gondwe.



Amesema serikali imetengeneza mfumo wa NaPA  ili kurahisisha huduma kwa wananchi hivyo unamhusu kila ambaye anafanya kazi serikali na asiye kwenye taasisi za serikali ambapo kwa watendaji wa kata mfumo huo utasaidia kupunguza siku za wananchi kupata huduma katika ofisi za kata.


"Tunafahamu sana mitandao ya kijamii kama vile Instagram,Tiktok ndio kama ilivyo NaPA na hii ni 'app' au 'soft wire' ambazo zimekuja kurahisisha huduma kwa watu mbalimbali hivyo tunaweza kusema tumetengenewa sehemu ya kukutana mtandaoni ili kupata huduma na wananchi kuhudumiwa haraka," amesema Gondwe.


Mkuu huyo wa Wilaya  ameongeza kuwa uzuri wa mfumo huu ni kwamba unakuwa ni rahisi kurejea kumbukumbu badala ya ngoja niende kwenye 'file'  lakini kupitia mfumo huu mtu anabofya tu matokeo yanatokea moja kwa moja.


Gondwe amesema mfumo wa NaPA pia utasaidia suala la ukusanyaji wa mapato kwa urahisi mfano kodi za majengo kwa kuwa idadi ya nyumba zitapatikana kutokana na Sensa na NaPA.


Ameongeza kuwa kwa upande wa biashara za mtandao, wafanyabiashara wanaofanya biashara zao mitandaoni itawarahisishia sana kuweza kufikisha bidhaa zao kwa wateja kirahisi na kuwajua wateja wao walipo.


"Badala ya kumwelekeza mtu kata kulia eeh hapa hapa angalia mti wa mbuyu kumbe mbuyu ulishakatwa zamani au angalia nyumba ya rangi ya kijani kumbe rangi ilishabadilishwa zamani,lakini kwa kutumia mfumo wa NaPA usumbufu wa kuelekeza hivyo hautakuwepo kwa kuwa mtu ataweza kuingia kwenye mfumo na kufika eneo husika kwa urahisi," amesema.


Amesema kutokana na umuhimu mkubwa wa Mfumo wa Anwani za Makazi kila mtumishi wa serikali na wananchi kwa ujumla wapakue 'app' ya NapA katika simu yake janja.


"Kwa maafisa Utumishi kwasababu serikali inatumia nyaraka za kielektroniki mtumishi anapohamishwa kupelekwa kituo kingine cha kazi wawe wanakabidhi pia nyaraka za kielektroniki ili kutowachanganya wananchi wanapokuwa wanapata huduma kupitia mfumo wa NaPA," amesema.


Naye Mratibu Msaidizi w Anwani za Makazi Kitaifa kutoka Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Arnold Mkude,amesema katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kumeanzishwa utaratibu wa utoaji wa barua ya utambulisho lengo ikiwa ni kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi wa kidigitali.


Amesema hatua iliyofikiwa ya utoaji wa barua ya utambulisho ni kwamba majaribio yameanza kufanyika kuanzia mwezi Machi hadi Mei 2024 ambapo wadau katika suala hilo ni watendaji wa kata,mitaa,vijiji,watoa huduma na wananchi na lengo la majaribio hayo ni kubainisha mapungufu na changamoto ili kuboresha kabla ya kuanza matumizi nchi nzima.


Mkude amesema tangu operesheni Anwani za Makazi ianze zimeweza kukusanywa taarifa za Anwani za Makazi milioni 12. 8 na zimewekwa nguzo za majina ya barabara zaidi 222,000 na vibao vya namba za nyumba zaidi ya milioni 4.


Amesema shughuli kuu zinazofanyika katika utekelezaji wa mfumo wa NaPA ni kusajili majina ya barabara na kutoa namba za Anwani za Makazi,kukusanya na kuhuisha taarifa za Anwani za Makazi,kuweka miundombinu ya mfumo,kutoa elimu na kuwajengea uwezo kwa watekelezaji na watumiaji wa mfumo.


"Kuna manufaa makubwa ambayo yamepatikana tangu kuanza kwa Mfumo wa Anwani za Makazi kwa mfano kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) matumizi yalipoanza Aprili 2023 katika suala la kukusanya kodi ya majengo kumesaidia kuongeza idadi ya maghorofa kutoka 4,164 hadi kufikia 32,000 na majengo ya kawaida kufikia 5,117,050 kutoka 2,988,546 yaliyokuwa yanatambulika awali kabla ya kuanza kwa mfumo huo.


Naye Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani ya Makazi kutoka Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Innocent Jacob, amesisitiza wananchi kuhakiki  anwani zao na kutumia program tumizi ya umma (NaPA) kujua anwani zao kwani anwani za makazi ni fursa katika shughuli za kijamii na kiuchumi.


Mratibu wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Mfumo wa Anwani ya Makazi kutoka Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Jampyoni Mbugi amesema utumiaji wa mfumo huo utasaidia sana utoaji wa huduma na kuondoa matukio ya kiuhalifu kwa kuwa kila mtu atajulikana alipo.


Naye Afisa Tehama, George Leonard, amesmea utaratibu wa utoaji wa barua za utambulisho utawarahisishia wananchi kupata huduma kwa njia ya mtandao.


Nao washiriki wa mafunzo hayo waliitaka serikali kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuhusu umuhimu wa Mfumo wa Anwani za Makazi ili waweze kuwa na uelewa mkubwa na kuutumia katika kupata huduma kwenye taasisi za serikali na zisizo za serikali.


















Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS