NA THABIT MADAI, ZANZIBAR
WAANDISHI wa Habari nchini wametakiwa kuandika habari za udhalilishaji na ukatili wa kijinsia kwa Wanawake na watoto kwa kuzingatia vigezo vya kiuandishi ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii dhidi ya vitendo hivyo.
Wito huo umetolewa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Salum Kassim Ali wakati akizungumza katika hafla maalum ya utoaji wa Tunzo za umahiri wa Uwaandishi wa habari za Takwimu iliyofanyika ukumbi wa Shaa Mjini Unguja.
Amesema kuwa, Takwimu zinaonesha kuongezeka kwa idadi ya vitendo vya udhalilishaji hivyo waandishi wa habari wanawajibu mkubwa kuendelea kuandika habari li kuchangia mabadiliko chanya katika jamii.
“Takwimu kutoka ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali zinaoesha kuwa, mwaka 2020 jumla ya matukio 1360 yameripotiwa, 2021 matukio 1361, 2022 matukio 1366 huku mwaka 2023 matukio 1994 yameripotiwa ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia,” ameeleza.
Ameongeza kuwa kwa mwezi wa Januari 2024 jumla ya matukio 1760 ya wanawake kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia yameripotiwa Zanzibar.
“Kiukweli idadi ni kubwa sana ya matendo haya ya udhalilishaji hivyo niwaombe ndugu zangu wanahabri kuongeza jitihada katika kuandika ili kuweza kupunguza haya matendo ambayo yanatia doa Zanzibar,” ameeleza.
Mapema Afisa kutoka Mamlaka ya kuia na Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) Yusuf Juma Suleiman ameahid mashirikiano baina ya ZAECA na Waandishi wa habari katika kutekeleza majukumu yao kila siku.
“Waandishi sis ZAECA tunaahidi mashirikiano na nyinyi kattika kutekeleza majukumu yenu hususani kuandika habari rushwa ya ngono ambayo nayo imekithiri,”ameeleza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Nchini Tanzania TAMWA Zanzibar Dkt. Mzuri Issa ameeleza kuwa, lengo la utoaji wa Tunzo hizo ni kushajihisha Waandishi wengi Zaidi kuandika habari za Wanawake na Uongozi pamoja na habari za kupinga udhalilishaji ili jamii iwe na uwelewa na kuondosha vitendo hivyo.
“Tunzo hizi zinaibua ari kwa waandishi vijana na Waandishi chipukizi ili kuandika habari ambazo zitaleta matukio chanya kwa jamii,” ameeleza.
0 Comments