Kamati ya Bunge ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na miongozo ya kitaifa kutoka nchini Uganda ikishirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano ya Uganda (NITA-U), imetembelea Ofisi kuu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili kujifunza mambo mbalimbali ya uendeshaji mamlaka hiyo.
Lengo kuu la ziara hiyo ni kujifunza jinsi Tanzania inavyosimamia sekta ya mawasiliano, ikihusisha mawasiliano ya simu, intaneti, utangazaji sanjari na huduma za posta.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Tony Ayoo (Mb) kutoka Uganda, wajumbe wa kamati wamepata fursa ya kujifunza namna TCRA inavyohudumia wadau mbalimbali katika sekta ya mawasiliano, ikiwemo wamiliki wa leseni, watumiaji wa huduma za mawasiliano na wadau wa sekta ya umma.
Wageni hao wamepokelewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA John Daffa, ambaye baada ya kuwakaribisha wabunge hao aliwapatia maelezo kuhusu majukumu ya TCRA na mchango wake katika kusimamia mawasiliano nchini.
“Jukumu letu ni kuhakikisha kwamba huduma zote zinazohusu mawasiliano, zilizo ndani ya ikolojia ya teknolojia ya habari na mawasiliano zinasimamiwa kwa ufanisi ili zichangie maendeleo ya nchi yetu” ameeleza Daffa.
Kamati hiyo pia imejifunza kuhusu namna TCRA inavyotekeleza majukumu yake ya kusimamia rasilimali muhimu za mawasiliano ikiwemo masafa ya mawasiliano, nambari za mawasiliano, kikoa cha taifa cha .tz na kanzidata ya anwani na postikodi.
Vilevile, wamejifunza kuhusu uboreshaji wa utoaji wa leseni za mawasiliano, ambazo sasa zinapatikana kwa njia ya mtandao kupitia jukwaa la Tanzanite, hivyo kuondoa ulazima wa waombaji kufika ofisini.
“Tumeweka mfumo wa utoaji leseni mtandaoni, unaorahisisha upatikanaji wa leseni kwa waombaji wapya na kupunguza changamoto za ufuatiliaji wa leseni kwa wawekezaji, maboresho haya yameleta ufanisi mkubwa katika usimamizi wa mawasiliano hapa nchini” amefafanua Kaimu Mkurugenzi wa TCRA.
Kuhusu upatikanaji wa teknolojia ya mawasiliano, Daffa amesema kwamba TCRA inahakikisha wananchi wanapata huduma za mawasiliano ya kasi na zenye ubora akitaja upatikanaji wa teknolojia ya mawasiliano ya simu kuwa umefikia asilimia 98 kwa 2G, 86% kwa 3G, 79% kwa 4G, na 10% kwa teknolojia ya 5G.
Wajumbe wa kamati hiyo kutoka Uganda wameipongeza TCRA na Serikali ya Tanzania kwa ujumla kwa mambo waliojifunza hususani usimamizi wa masafa ya utangazaji wa Redio, usimamizi wa kikoa cha Taifa cha .tz, utangazaji wa Redio kidijitali na jinsi Tanzania inavyowezesha vijana kushiriki katika uchumi wa kidijitali.
0 Comments