Header Ads Widget

ALICHOANDIKA JOHN MNYIKA KUHUSU KIFO CHA MZEE RUKSA

  


Nimepokea kwa mchanganyiko wa masikitiko na shukrani kwa Mwenyezi Mungu taarifa ya kifo cha Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi.


Masikitiko kwa kuwa hatutakuwa naye kimwili lakini shukrani kwa kuwa Mungu ameitwaa roho yake akapumzike baada ya utumishi na umri mrefu aliomjalia.


Mambo manne tumuenzi nayo: Mosi, tukamilishe mageuzi ya kiuchumi. Wakati anakuwa Rais wa pili nchi ilikuwa katika hali ngumu ya kiuchumi. Akahitimisha majadiliano na nchi hisani na mashirika ya kimataifa na kuunda timu iliyotoa mapendekezo ya Mageuzi ya Uchumi (Economic Reform Programmes 1 and 2). Hatua mbalimbali zikapigwa. Rais Mwinyi amefariki fedha za kigeni zikiwa adimu, hali ya uchumi iko tete yenye kuhitaji mageuzi mengine makubwa. Tumuenzi kwa kufanya mageuzi hayo ambayo pamoja na mambo mengine yatainua uchumi wa watu wengi na kupunguza bei ya bidhaa muhimu na ugumu wa maisha kwa wananchi.


Pili, tukamilishe mageuzi ya kisiasa . Mzee Mwinyi alishika Urais wakati dunia ikiwa kwenye wimbi la kutoka mfumo wa siasa wa Chama kimoja kuingia mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Aliunda Tume ya Nyalali 1991 na hatimaye Tanzania ikarejesha mfumo wa vyama vingi 1992. Hata hivyo, hatua hiyo haikuambatana na mageuzi ya kikatiba na kisheria ya kuweka misingi ya haki, uhuru na usawa ya demokrasia ya vyama vingi na taasisi imara za kikatiba katika taifa. Tumuenzi kwa kuendeleza mchakato wa kupata #KatibaMpya na #ChaguziHuruNaHaki .


Tatu, tupate muafaka wa kitaifa kuhusu muundo wa muungano Tanganyika na Zanzibar na mfumo wa utawala wa Tanzania. Katika utawala wa Mzee Mwinyi palitokea mzozo kuhusu mfumo wa utawala wa Tanzania mintaarafu muundo wa muungano. Fukuto ya jambo hili lilikuwepo kabla na lipo hata sasa. Mchakato wa mabadiliko ya katiba na maoni yaliyokusanywa na Tume ya Warioba yalikuwa yanatupeleka kwenye muafaka wa kitaifa, hata hivyo kuvurugwa kwa mchakato kwenye Bunge Maalum la Katiba 2014 kumeliacha taifa katika mkwamo juu ya suala hilo tete na tata. Tumuenzi kwa kuendeleza mchakato mpaka muafaka wa kitaifa upatikane tuwe na mfumo mpya wa utawala.


Nne, tuendelee kuikuza lugha adhimu ya Kiswahili. Baada ya Nyerere Mzee Mwinyi alikuwa kinara katika hili. Kwa kuwa lugha ya Kiswahili sasa inatambulika kimataifa. Ni wajibu wetu wa kushawishi iwe lugha kuu ya Afrika na iwe moja ya bidhaa na huduma za Tanzania na Afrika Duniani katika masoko ya kiuchumi, medani za siasa, ushindani wa kiutamaduni, mwingiliano wa kijamii na utandawazi wa kimtandao na kidigitali. Ni vyema kukawa na mkakati mahususi kuhusu suala hili chini ya Rais wa sasa.


Poleni sana familia ya Mzee Mwinyi, poleni sana watanzania. Mwenyezi Mungu aijalie roho ya Ali firdaus. Inna lillahi wa inna ilalhi raji'un 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI