Na Shemsa Mussa,Kagera
Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilayaya Karagwe Mkoani Kagera
limeiomba Serikali kuingilia kati ili kuona namna ya kuwasaidia Wananchi na Viongozi wake kupata muafaka katika uwekezaji wa mradi unaoendelea wa upanuzi wa kilimo cha miwa unaofanywa na kiwanda cha Sukari (Kagera Sugar) Wilayani Misenyi Mkoani Kagera kwenye eneo la ardhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ili wapate chochote kinachoingia kama mapato ya Halmashauri hiyo.
Hoja hiyo iliibuliwa na Madiwani wa Halmashauri hiyo baada ya kuhojiwa na Wananchi wengi juu ya nini kinaingizwa kutoka katika eneo hilo kubwa la uwekezaji ikiwa liko katika eneo la Halmashauri hiyo ndipo madiwani hao kwa pamoja waliamua kujadili na kuona njia nzuri ni kuikimbilia na kuiomba Serikali ili ione namna ya kuingilia suala hilo nyeti na haki kupatikana.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Wallece Mashanda akizungumza katika kikao maalum cha Baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Angaza uliopo mjini Kayanga Wilayani humo alisema kuwa anawapongeza sana Kagera Sugar kwa uwekezaji huo wa kupanua kilimo cha miwa kutokana na kulima eneo kubwa ambalo linaendelea kupanuliwa lakini kwa upande wa pili imeonekana kwa kipindi sasa kumekuwepo mvutano juu ya uwajibikaji katika suala la kulima eneo hilo na kulitumia likiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.
"Eneo hilo ni kubwa na Kuna athari fulani za kimazingira zimetokea ambazo zimewagusa Wananchi moja kwa moja lakini hakuna kitu chochote kinachoingia katika Wilaya yetu kama mapato jambo hili linaleta maumivu kwa Viongozi kutokana na kutopata muafaka wa eneo hili juu ya kinacholipwa" alisema Mashanda.
Mashanda aliongeza kuwa kuna haja ya wenye mradi huo kutumia busara kwa kuona kazi iliyofanyika na eneo kubwa lililochukuliwa na lilivyotumika miti iliyokatwa hivyo izingatie kuwa Wananchi wa Karagwe na Halmashauri yao wana haki ya kupata kitu chochote hivyo lazima uwajibikaji wa mapato yake uwepo.
Aidha akizungumza kwa uchungu baada ya hoja hiyo kuibuliwa Diwani wa Kata ya Kayanga Germanus Byabusha alisema lazima waone ni namna gani watafaidika na kuwa leo hii hamna haja ya kuanza kukimbizana na Wananchi wa kawaida katika magurio kwa shilingi mia mbili za ushuru wakati kuna uwekezaji huo mkubwa katika eneo lao.
"Kama alivyoelekeza Mwenyekiti wa Halmashauri yetu pamoja na Mkuu wa Wilaya yetu ya Karagwe katika kikao kilichopita ni lazima Viongozi hao wakae wazungumze vizuri na Mbunge na kuna haja pia Waziri wa kilimo kubadili sheria za sukari" alisema Diwani huyo.
Hata hivyo aliongeza kuwa ni lazima haki ipatikane ili kuwapunguzia mzigo Wananchi na kuleta maendeleo hivyo wanatakiwa wapate chochote kwani ni haki yao.
0 Comments