Header Ads Widget

WAZIRI AMWAGA SIFA KWA WANAHARAKATI WA KUPAMBANA NA VITENDO VYA UDHALILISHAJI

 

NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR 

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Riziki Pembe Juma, amesema, wanaharakati wanamchango mkubwa katika kupinga vitendo vya udhalilishaji na kuwataka kupiga vita hasa katika eneo la udhalilishaji ili kuona Taifa linabaki katika hali nzuri.


Akizungumza katika hafla ya kuwakabidhi Tunzo wadau mbalimbali wa kupinga vitendo vya udhalilishaji pamoja na waandishi wa habari waliofanya vizuri katika masuala hayo katika shindano lililoandaliwa na Jumuiya ya wanasheria wanawake Zanzibar (ZAFELA), ikiwa ni miongoni mwa sherehe ya kutimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo, hafla ambayo ilifanyika katika ukumbi wa Golden Tulip ya Uwanja wa ndege Mjini Unguja.

Alisema viongozi wa nchi wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha matendo hayo yanaondoka hivyo ni vyema wanaharakati kuendelea kupigana ili kuhakikisha vinapungua na kuondoka kabisa.


Aidha alisema wanaharakati kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakipambana na  kuona wanakemea vitendo vya udhalilishaji sambamba na kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto na kwa wanawake.


Alisema serikali inaelewa kuwepo kwa changamoto nyingi wanazokumbana nazo wanaharakati ambapo imekuwa inafikia wakati wanakata tamaa hivyo aliwasisitiza kutokata tamaa na kuwataka kuendelea na mapambano zaidi kwa maslahi ya Taifa.

‘Tuhakikisheni kuwa tunaendelea kulisaidia Taifa, tunawasaidia watoto, wanawake na jamii na vizazi vyetu vilivyopo sasa na vinavyokuja huko mbele kwani waliopo hivi sasa ni viongozi wa kesho na ndio wazazi wa kesho’ alisema .


Hivyo, aliwataka wadau hao kila mmoja kupaza sauti yake kwa namna anavyoweza kwa utaratibu uliokuwa mzuri katika kuhakikisha wanapiga vita vitendo vya ukatili wa jinsia kwa watoto na wanawake.


Sambamba na hayo, aliipongeza jumuiya ya ZAFELA kwa kutimiza miaka 20 na kuwataka kuendelea kufanya kazi ikiwemo ya kutatua changamoto za wananchi katika kujua haki zao zinazowakwaza ikiwemo kesi za udhalilishaji ambao ni tishio kwa wananchi kwa sasa.

Hata hivyo, aliwapongeza wadau wote waliopata tunzo na kuwasisitiza kuendelea kupambana zaidi ili kuona vitendo hivyo viweze kuondoka nchini


Mapema, Mkurugenzi wa Jumuiya ya wanasheria wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jamila Mahmoud, alisema, Tunzo hizo zimetolewa kutokana na mchango wao wanautoa katika jamii hasa katika kuona vitendo vya udhalilishaji vinaondoka.

Aidha alisema kwa mwaka huu Tunzo zilizoingia katika kinyang’anyiro ni 12 ikiwemo Tunzo moja  maalum ambayo imetolewa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuthamini jitihada za wanaharakati.


Nao, washiriki wa Tunzo hizo, wameahidi kuendelea kupambana na kuhakikisha masuala ya udhalilishaji vinapungua na kuondoka kabisa nchini.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI