Na,Jusline Marco;Arusha
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Dunstan Kitandula amesema Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) ina mchango mkubwa katika sekta ya uhifadhi wa malisili na uboreshaji wa biashara ya utalii nchini.
Kitandula ameyasema hayo wakati alipotembelea ofisi za makao makuu ya Taasisi hiyo zilizopo katika Eneo la Njiro jijini Arusha na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi na Menejimenti ya TAWIRI ambapo amesema tafiti za TAWIRI zinamchango mkubwa katika sekta ya uhifadhi na utalii nchini.
Aidh Kitandula amewapongeza wataalamu wa TAWIRI kwa umahiri na ubobevu, ambao umewaleta wadau kutoka nchi mbalimbali kuja kupata uzoefu katika nyanja mbalimbali ikiwemo sensa za wanyamapori.
"niwapongeze kwa umahiri wenu, kwani mnashiriki kukuza utalii kupitia zao jipya la utalii wa utafiti " amepongeza Dkt. Kitandula.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi TAWIRI, Dkt.David Manyanza amesema bodi hiyo na wataalam kupitia mpango mkakati utakaohuishwa, imeandaa vipaumbele vitakavyoongeza wigo wa Taasisi hiyo kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kisayansi kwa wakati ili kuimarisha uhifadhi na kukuza utalii nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI Dkt. Eblate Ernest Mjingo amesema mbali na taasisi hiyo kuwa na wataalam mahiri, inatumia teknolojia za kisasa katika tafiti ikiwa ni matumizi ya visukuma mawimbi kuwafuatilia wanyamapori, matumizi ya akili mnambe katika kufanya sensa ya wanyama.
0 Comments