Header Ads Widget

SHIRIKA LA BRAC MAENDELEO LAWAPIGA TAFU WAJASIRIAMALI 902 WANAWAKE

  

SHIRIKA LA BRAC MAENDELEO LAWAPIGA TAFU WAJASIRIAMALI 902 WANAWAKE 


Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA


SHIRIKA lisilo la kiserikali la Brac Maendeleo Tanzania (BMT)  limetoa msaada wa vyerahani,vifaa vya saloon, kuku, ng'ombe, mbuzi na vifaa vya umwagiliaji kwa wajasiriamali 902 wa Wilaya za Manyoni na Singida vyenye thamani zaidi ya Sh.milioni 303.7 ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.


Meneja wa Mkoa wa shirika hilo, Isihaka Mirambo alisema vitu hivyo vimetolewa na shirika kupitia mradi wake wa Kuwawezesha Wanawake na Mabinti Barehe Kiuchumi (AIM) baada ya wanawake hao kupewa mafunzo ya stadu za maisha ambayo walisajiluwa washiriki 2400 lakini walioshiriki mafunz0 hadi mwisho ni 902.


Alitoa mchanganuo kuwa vyerahani watapewa wajasiriamali 226,seti za salooni watu 70, kuku 175 ambayo kila mmoja atapewa kuku 10 pamoja na dawa, ng'ombe 50 , mbuzi watapatiwa watu 85 kwa kika mmoja mbuzi watatu,vifaa kwa ajili ya kuendesha kilimo cha umwagiliaji ambavyo watanufaika wanawake 35 na utengenezaji sabuni.



Aidha,wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wapatao 180 wamenufaika kwa kupewa vifaa vya shule ambavyo ni mabeji,madaftari (counter book),kalamu,penseli na sare za shule.


Mirambo alisema Brac Maendeleo Tanzania imetoa vitu hivyo ikiwa ni mkakati wa shirika hilo kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kugusa maeneo ambayo serikali haijayafikia ili kuwainua wananchi kiuchumi.


Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida,Dk.Fatuma Mganga ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa ugawaji wa vifaa hivyo kwa wanawake, alilishukru Shirika la Brac Maendeleo Tanzania kwa jinsi lilivyojipambanua kwa dhati kuondoa umasikini kwa wananchi hususani wanawake wa mkoani hapa.


"Kupitia mradi huu Brac Maendeleo Tanzania sasa wanawake mnakwenda kuwasaidia akina baba majukumu ya kifamilia kwasababu una saloon yako unaweza ukawa unaingiza hata Sh.20,000 kwa siku ila usizitumie zote unaweka akiba zitakusaidia baadaye maana akina baba shida zikizidi huwa wanakimbia familia sasa akikimbia wewe huna presha," alisema.


Dk.Mganga alisema suala la kupewa vifaa hivyo ni jambo moja na kuvitumia ili vizalishe ni jambo jingine hivyo ni jukumu la kila mwanamke aliyepewa vitu hivyo kujitambua,kujituma,kujitoa, kuvitumia na kujiwekea akiba ili viweze kuleta matokeo chanya.




"Leo tunapewa vifaa hivi sitegemei vifaa vinakwenda kukaa mwezi mzima nyumbani kama mapambo nina imani kila mtu atatafuta sehemu nzuri ya kufanyia shughuli zake,hatutegemei mtu aje na hadithi kwamba ameibiwa na atakayefanya uzembe vikaibiwa tutamchukulia hatua," alisema.


Aliongeza kuwa ni marufuku kwa mwanamke yeyote aliyepewa vifaa hivyo kuviuza na kuwagiza maafisa maendeleo kuwafuatilia wanufaika wote kujua kama wanaendelea kuvitumia na kuwasaidia kutafuta wateja badala ya kuwaacha tu kama picha.


Alisema kila mnufaika aweke mpango kazi wake wa biashara kwa kutumia elimu ya ujasiriamali waliyofundishwa na kuonya wanawake watakapoanza kupata pesa wasizitelekeze familia zao.



"Baadhi ya wanawake wakishaboreka kiuchumi tunaanza kuleta dharau katika familia,huu mradi tuliopewa sio kwenda kuvunja familia,busara na hekima ni pale unaimarika kiuchumi na kuendelea kumheshimu mume wako na kutunza familia yako," alisema.


Nao Latifa Yohana na Emmy Gervas wakizungumza kwa niaba ya wanufaika walilishukru Shirika la Brac Maendeleo Tanzania kwa msaada huo na kuahidi kuvitumia vifaa hivyo kuboresha maisha yao kiuchumi.


MWISHO

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI