Header Ads Widget

MADIWANI MKALAMA WALIA KIFUTA JASHO KIDOGO WANACHOLIPWA WAATHIRIKA WA TEMBO

 



Na Thobias Mwanakatwe, Mkalama


MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida wameitaka serikali kuifanyia mabadiliko sheria ya malipo ya fidia kwa wananchi ambao mazao yao yanaharibiwa  na tembo mashambani  kwani kiwango kinachotolewa kwa waathirika ni kidogo sana ukilinganisha na athari wanazopata.


Diwani wa Kata ya Mwangeza,Bosco Samweli, akizungumza juzi kwenye kikao cha robo ya kwanza cha kujadili utekelezaji wa miradi, alisema maeneo mbalimbali katika Wilaya ya Mkalama wananchi wamekuwa wakikubwa na uvamizi wa tembo kwenye nyumba zao na uharibifu wa mazao mashambani.


Mwangeza alisema lakini kiwango cha Sh.100,000 kinachotolewa kwa waathiriwa wa mashamba na Sh.1,000,000 kinachotolewa kama kifuta jasho kwa wanaopoteza maisha ni kidogo sana hivyo kuna haja ya kubadili sheria ili kiwango cha malipo ya fidia na kifuta jasho kiongezeke.


Diwani wa katabya Kikhonda,Elisha Kanka, alisema suala la upatikanaji wa vitambulisho vya taifa limekuwa kero sana kwa wananchi na kuitaka serikali isogeze huduma za vitambulisho hivyo karibu na wananchi.


Naye Diwani wa kata ya Nkinto, Reuben Charles alisema mbegu za  alizeti za ruzuku zinazotolewa na serikali kwa mfululizo wa miaka miwili ya msimu wa kilimo zimekuwa na hazistawi vizuri jambo linalowakatisha tamaa wananchi.



Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama,Abdalla Njelu,akijibu hoja ya tembo  alisema ni kweli wilaya hiyo wananchi wanapata sana changamoto ya tembo na kwamba suala la kutaka kiwango cha malipo na fidia na kifuta jasho kiongezwe wataliwasilisha katika ngazi husika.


Katika hatua nyingine Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida imeadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake huku mafanikio lukuki yakielezwa yakiwamo kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato kutoka Sh.milioni 247 zilizikusanywa katika bajeti ya 2013/2014 hadi kufikia Sh.bilioni 1.749 ambazo zinazokusanywa hivi sasa.


Kaimu Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya Mkalama,Daniel Tesha,akielezea juzi mafanikio hayo katika maadhimisho yaliyowashirikisha madiwani,watendaji wa vijiji na kata,wakuu wa idara na viongozi wa serikali, alisema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na ushirikiano mzuri wa watumishi katika halmashauri hiyo.


Tesha alisema katika kipindi cha miaka 10, halmashauri hiyo imepata hati safi mfululizo miaka tisa na hati moja yenye mashaka. Wilaya Mkalama ilianzishwa Julai 2012 baada ya kumegwa kutoka Wilaya Iramba.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI