Na WILLIUM PAUL,
SERIKALI imeshafanya tathimini ya uwekaji wa umeme katika hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Moshi iliyopo kata ya Mabogini jimbo la Moshi vijijini ili mpaka ifikapo January 2024 kuwe na umeme wa uhakika.
Hayo yamekuja siku chache baada ya wananchi wa kata hiyo kuishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kujenga hospitali hiyo ya wilaya katika kata hiyo hali ambayo itawaondolea hadha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya katika hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Mawenzi.
Akiuliza swali Bungeni jana, Mbunge wa jimbo la Moshi vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi alisema kuwa, hospitali mpya ya wilaya iliyopo kata ya Mabogini imeanza kutoa huduma je serikali inampango gani wa kupeleka umeme katika hospitali hiyo mpya.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga alisema kuwa, hospitali hiyo imeshafanyiwa tathimini na wapo katika mchakato wa kupata fedha ili ifikapo Januari 2024 iwe imeshapata umeme wa uhakika.
Majibu hayo yamepokelewa kwa furaha kubwa na wananchi wanaotumia hospitali hiyo ambapo wamempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hasan na Mbunge wa jimbo hilo Profesa Patrick Ndakidemi kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakiwajali na kuwapambania.
Mwisho...
0 Comments