Na Mbaruku Yusuph Matukio Daima APP, Handeni.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM)kimewaasa wataalam na watumishi wa Serikali wafanyekazi kwa weledi na chama hicho hakitakuwa tayari kuwavumilia watumishi watakaokaidi na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa Tanga Rajabu Abdurahman alipohudhuria dua ya kumuombea Rais Samia iliyofanyika Wilayani Handeni katika kata ya Kwamagome ambapo viongozi mbalimbali wa chama na Serikali walihudhuria.
Rajabu ambae alikuwa mgeni rasmi katika ghafla hiyo alisema amekuwa na ziara ya siku tatu katika Wilaya za Tanga Mjini, Muheza,Pangani na Handeni ambapo aliambatana na kamati ya Siasa ya Mkoa,ziara iliyolenga kuendelea kukagua utekekezaji wa ilani ya chama hicho na kusikiliza kero za wananchi.
Alisema katika ziara hiyo amekagua miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayotekelezwa na Serikali na ile inayotekelezwa na mashirika yasiyo ya kiserikali ambapo baadhi ya miradi hiyo usimamizi wake hauridhishi jambo ambalo lilimpelekea kutoa maelekezo kwa watumishi wa Serikali na Chama.
"Sisi kama chama hatutakuwa tayari kumvumilia mtumishi atakaetukwamisha na niweke wazi tu fedha za Serikali haziliwi na tukikubaini tutamshauri Rais nini afanye"Alisema Ndugu Rajabu.
Ndugu Rajabu alisema kumuunga Mkono na kumsaidia Rais ni kufanyakazi kwa weledi sambamba na kusimamia vema miradi ya maendeleo na fedha zinazotumwa kwa kila Halmashauri lazima zitumike kama ilivyokusudiwa na si vinginevyo.
Alisema wakati umefika kwa kila mtumishi wa Serikali na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi wahakikishe miradi na shughuli zote za kimaendeleo zinatekelezwa kwa wakati na ziendane na thamani halisi ya fedha zilizotengwa.
"Labda nitoe mfano Handeni mmepata Shs Mil 900 kama wenzenu wa Pangani na mkaona Mil 400 mjenge Jengo la wagonjwa wa dharura na Shs Mil 500 ndio mkarabati majengo ya zamani wazo zuri sana lakini jengo hilo limechukua muda mrefu na ninamashaka na ubora wake haya ndio mambo Rais asiyoyataka lazima tuchukue hatua"Alisema ndugu Rajabu.
Alitumia fursa hiyo kuwaagiza watumishi wote wa Serikali na Viongozi wa Chama Mkoani Tanga washirikiane kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wakati na iendane na thamani halisi ya fedha zilizotengwa na kufanya hivyo ndio kumsaidia Rais Samia kutimiza azma yake ya kupunguza kama si kumaliza kero za mwananchi
Kwa upande wake Diwani wa kata ya kwamagome Musa Mkombati alisema ghafla ya Dua hiyo imetokana na Rais Samia kuwa mstari wa mbele kupigania maendeleo ya wananchi wake na kupambana kuwaondolea kero zinazo wakabili wananchi hao.
Mkombati ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Handeni Mji alisema wananchi na wanafunzi walikuwa wanatembea umbali mrefu kufuata huduma ya Afya,maji na elimu na walitembea umbali wa zaidi ya km 34 kufuata huduma hizo jambo ambalo limetatuliwa kwa kiasi kikubwa.
"Tuna kila sababu ya kufanya Dua kwa ajili ya Rais wetu ametupa pesa kwa ajili ya miradi ya maji,shule,Hospitali, vtuo vya afya,umeme n.k na kwa kufanya hivyo amesaidia wananchi kutokutembea umbali mrefu kama hapo awali"Alisema Mkombati.
0 Comments