Washiriki wa mkutano huo wa siku moja kutoka mikoa ya Mbeya,Songwe,Mbeya,Iringa,Njombe,
Na Matukio Daima Media, Mbeya
WAZAZI na walezi wametakiwa kutambua mapema mabadiliko ya kitabia kwa watoto wao ili kuwa na kizazi ambacho hakitaiga tabia hatarishi kutoka mataifa ya nje.
Hayo yameelezwa na mratibu wa elimu ya afya kwa umma mkoa wa Mbeya ,Mashaka Juma katika kikao kazi cha mradi wa utafiti unaolenga kuangalia uwezo wa taasisi katika kuratibu afua za mawasiliano na mabadiliko ya tabia ya jamii kwenye ukumbi wa Hoteli ya Usungilo jijini Mbeya.
Amesema kutokana na utandawazi uliopo kwa sasa ni wakati muhimu kwa wazazi na walezi kuwa waangalifu katika suala la malezi.
"Ni wakati muhimu kwa wazazi na walezi kujikita zaidi kwenye uangalizi wa watoto wao kutokana na utandawazi uliopo hivi sasa ambao unaweza kuharibu watoto na hata kutoiga mifumo ya kiutandawazi ambayo inaweza kuwa hatarishi kwa kizazi kilichopo na kijacho"amesema Mashaka.
Kwa upande wake Afisa maendeleo ya jamii Halmashauri ya wilaya ya Mbeya,Agnes Elikunda amesema kunahitajika ubunifu zaidi katika kubadili tabia kwenye jamii .
Hata hivyo Elikunda ameitaja mbinu ya Uraghabishi kama njia rahisi inayoweza kutumika kuleta mabadiliko ya tabia katika jamii.
Mkutano huo wa siku moja umewakutanisha Wataalamu mbalimbali wa serikali, asasi za kiraia na vyombo vya habari kutoka mikoa ya Mbeya,Iringa,Njombe na Songwe.
Mwisho.
0 Comments